TANZANIA MWENYEJI MKUTANO WA KWANZA WA AFRIKA KUHUSU MATUMIZI ENDELEVU YA ZANA ZA KILIMO
Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) katika hotuba yake, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumwamini kuongoza Wizara ya Kilimo katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambapo kilimo kipo kwenye Sekta muhimu za mageuzi ya Taifa.
Amesema hayo wakati akimkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), wakati wa uzinduzi wa Mkutano wa Kwanza wa Afrika kuhusu Matumizi Endelevu ya Zana za Kilimo (Africa Conference on Sustainable Agricultural Mechanization - ACSAM) tarehe 3 Februari 2026, katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam.
Akisoma hotuba yake, Mhe. Chongolo amewashukuru Mawaziri wa Kilimo kutoka Nigeria, Somalia, Niger, Afrika ya Kati, Rwanda, na Senegal kwa kushiriki katika mkutano huu na kusema kuwa mkutano umewaunganisha watunga sera, wawakilishi wa Serikali, wadau wa maendeleo, watafiti, wakulima, asasi za kiraia, na Sekta Binafsi ili kubadilishana uzoefu na kupata mbinu bora za kuimarisha matumizi endelevu ya Zana za Kilimo.
Mkutano wa ACSAM umeanzishwa kama jukwaa la kipekee la kubadilishana mbinu bora, kukuza ushirikiano wa kikanda, na kuhimiza matumizi endelevu ya zana za kilimo zinazochangia kuongeza tija na kipato kwa wakulima barani Afrika.