Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

TANZANIA NA ALGERIA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KILIMO

Imewekwa: 04 Aug, 2026
TANZANIA NA ALGERIA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KILIMO

Tanzania na Algeria zimekubaliana kuimarisha Sekta ya Kilimo nchini kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kuongeza tija na kuendeleza wakulima wadogo kupitia uzalishaji na biashara endelevu katika soko la Algeria.

Hayo yamejadiliwa kati ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) na Balozi wa Algeria nchini Tanzania, Mhe. Ghalib Zermane tarehe 03 Julai 2026, katika ofisi za Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), jijini Dar es Salaam. 

Majadiliano hayo yameangazia fursa za biashara na uwekezaji, matumizi ya teknolojia za kisasa za kilimo na kuongeza thamani ya mazao, hususan katika tasnia za Kahawa na Ndizi. 

Tanzania imekuwa ikiuza Kahawa katika masoko ya kimataifa kutokana na ubora wake na mfumo wa kisayansi wa upangaji wa madaraja, ambao hupunguza vihatarishi vya biashara na kuongeza ushindani wa kimataifa. 

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Zermane amebainisha kuwa Algeria ni soko kubwa la bidhaa za kilimo, ikitumia takribani tani 130,000 za Kahawa kwa mwaka zenye thamani ya kati ya Dola za Marekani Milioni 600 hadi 700.  Vilevile, matumizi ya Ndizi nchini humo hufikia takribani tani 250,000 kwa mwaka zenye thamani ya takribani Dola za Marekani Milioni 250.  Takwimu hizi zinaonesha kasi ya ukuaji wa soko la Algeria na kuongezeka kwa uagizaji wa bidhaa hizo katika miaka ya hivi karibuni.

Viongozi walioshiriki katika mazungumzo hayo ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu Bw. Samuel Mshote wa TFC; Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania Bw. Primus Kimaryo; Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao katika Wizara ya Kilimo, Dkt. Yasinta Nzogela; Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).