Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

TANZANIA NA AUSTRALIA KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA KILIMO

Imewekwa: 12 Jun, 2025
TANZANIA NA AUSTRALIA KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA KILIMO

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Australia nchini Tanzania, Mhe. Jenny Da Rin, tarehe 9 Juni 2025 kuhusu ushirikiano katika Sekta ya Kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji nchini. 

Mhe. Waziri Bashe amebainisha maeneo muhimu ya ushirikiano ambayo ni pamoja na utafiti hasa katika zao la ngano ili kupunguza uingizaji wa zao hilo kutoka nje ya nchi.

Amesisitiza umuhimu wa nchi hiyo kushirikiana na Taasisi za utafiti nchini ikiwemo TARI katika masuala ya utafiti pamoja na uzalishaji mbegu.  Ameeleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada katika kuhakikisha miundombinu bora ya uhifadhi wa mbegu kupitia Benki ya vinasaba vya mbegu inakuwepo katika kuhakikisha usalama wa chakula nchini.

Aidha, Mhe. Waziri Bashe ameainisha eneo la zana za kilimo pamoja na umwagiliaji kama maeneo ya uwekezaji na kuikaribisha Serikali ya Australia kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) na Tanzania katika maeneo ya Sekta ya Kilimo ili kurahisisha ufanisi na kuondoa mkanganyiko wa eneo moja kufadhiliwa na wafadhili wengi kwa wakati mmoja.

Tanzania na Australia wamekuwa na historia ya ushirikiano katika Sekta ya Kilimo ambapo Australia imekua ikinunua kahawa kutoka Tanzania na huku Tanzania ikinunua ngano.  Hivyo, Mhe. Waziri Bashe alitoa rai kwa wawekezaji wakubwa kutoka Australia kuwekeza katika zao la kahawa hapa nchini.