TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA KUHAMASISHA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA KILIMO NA CHAKULA BARANI AFRIKA
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb), ameshiriki kikazi katika Mkutano wa Kuhamasisha Sekta Binafsi kwa Biashara Endelevu na Uwekezaji katika Sekta ya Chakula Barani Afrika, jijini Nairobi nchini Kenya.
Mkutano huo umeandaliwa kwa pamoja kati ya Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) na Serikali ya Jamhuri ya Kenya na kufunguliwa na Mhe. William Kabogo (Mb), Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Kidigiti wa Kenya. Washiriki wengine ni pamoja no Makamu wa Rais Mstaafu wa Nigeria; Mawaziri wa Kilimo kutoka Barani Afrika na nchi ya Romania; wakiwemo wawekezaji kutoka Umoja wa Ulaya.
Naibu Waziri Silinde ameshiriki mjadala uliohusu matumizi ya akili mnemba (AI) na teknolojia za kidigiti katika kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi na maji katika Sekta ya Kilimo na chakula Barani Afrika. Akichangia mada hizo, Mhe. Silinde aIielezea hatua mbalimbali ambazo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo imechukua katika kuongeza matumizi ya teknolojia za kidigiti akitolea mfano wa kufanikiwa kuwa na mfumo wa kusajili wakulima, usimamizi wa ruzuku ya pembejeo na takwimu za kilimo.
Amefafanua zaidi kuwa matumizi ya akili mnemba yanawezesha Serikali kutabiri mwenendo wa uzalishaji, kutabiri mahitaji ya soko na taarifa za biashara ili mkulima kujipanga ipasavyo katika uzalishaji na uuzaji wa mazao. Mhe. Silinde pia ameeleza kuwa matumizi ya akili mnemba yanawezesha pia kuunganisha data ya uzalishaji wa kilimo na taarifa za hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ili kutengeneza mifumo ya tahadhari ya mapema kwa ukame na mafuriko, kuboresha ustahimilivu na mipango ya kilimo kwa wakulima.
Aidha, Naibu Waziri Silinde alichangia kuhusu mifumo ya utoaji vibali iliyotengenezwa katika Sekta ya Kilimo ambayo imekuwa ikirahisisha huduma za biashara ya mazao ya kilimo kwa wadau waliopo ndani ya nchi na nje ya nchi.