Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

TARI YATAKIWA KUONGEZA KASI UJENZI WA OFİSİ NA KUZINGATIA UBORA

Imewekwa: 09 Jun, 2026
TARI YATAKIWA KUONGEZA KASI UJENZI WA OFİSİ NA KUZINGATIA UBORA

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imekaliwa kuongeza kasi ujenzi wa Ofisi za Utawala zinazojengwa katika eneo la Mtumba, jijini Dodoma ili kuongeza ufanisi zaidi katima utekelezaji wa majukumu yake. 

Akikagua maendelel ya ujenzi huo tarehe 9 Juni 2026, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Athumani Kilundumya alipata fursa ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo na kujionea maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo la kisasa lenye ghorofa tano, ambalo linatarajiwa kuwa Makao Makuu ya shughuli za utawala za taasisi hiyo.

Mradi huo unafadhiliwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo (ADF) na utekelezaji wake ulianza rasmi Januari 30, 2026. Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa wakati wa ukaguzi huo, ujenzi umefikia asilimia 20 na unaendelea kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa.

“Nimefarijika kuona maendeleo mazuri ya ujenzi huu.  Nawapongeza TARI na timu nzima ya usimamizi wa mradi kwa juhudi wanazozionesha katika kuhakikisha mradi huu muhimu unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa,” amesema Mha. Kilundumya.

Amewataka wahandisi na wasimamizi wa mradi huo kuongeza kasi katika ujenzi kwa kuhakikisha unakamilika kwa ufanisi, ubora na wakati uliopangwa na, ikiwezekana, kabla ya muda uliobainishwa kwenye mkataba.

Amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha mazingira ya kazi kwa Watumishi wa TARI na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo ya kufanya tafiti za kilimo kwa ajili ya maendeleo ya Sekta ya Kilimo nchini.  Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2027.