TFSRP YATOA MAFUNZO YA UTUNZAJI WA MAZINGIRA, MATUMIZI SAHIHI YA VIUATILIFU NA JINSIA KATIKA VITUO VYA UTAFITI WA KILIMO
Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) inayotekelezwa na Wizara ya Kilimo imetoa mafunzo maalum kwa Watafiti, Maafisa Kilimo, Wakulima na wafanyakazi wa kada zote katika Vituo vya Utafiti vya Kilimo vilivyopo chini ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kuanzia tarehe 16 hadi 20 Februari 2026.
Lengo kuu ni kujenga uelewa juu ya umuhimu wa kujumuisha masuala ya mazingira ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya viuatilifu, afya na usalama mahala pa kazi, masuala ya jinsia na ukatili wa kijinsia, namna ya kupokea na kushughulikia malalamiko/maoni/maswali pamoja na usimamizi bora wa taka zinazozalishwa ili kupunguza madhara katika mazingira.
Mafunzo hayo yamelenga kuhakikisha watekelezaji wote wa Program ya TFSRP wanapata uelewa wa kina na kuzingatia maelekezo yaliyowekwa katika kipindi chote cha utekelezaji, kwa lengo la kuboresha uhimilivu wa uzalishaji katika sekta ya kilimo dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, kulinda na kusimamia rasilimali za msingi za uzalishaji, pamoja na kuimarisha upangaji na utekelezaji wa sera na mikakati ya Sekta ya Kilimo.
Aidha, mafunzo hayo yanasisitiza umuhimu wa tafiti kuzingatia mifumo ya kitaifa ya usimamizi wa mazingira, kuhakikisha masuala ya uwezeshwaji na ujumuishwaji wa kijinsia yanapewa kipaumbele, na kujenga uwezo wa kupokea na kushughulikia malalamiko, maoni na maswali yanayohusu utekelezaji wa Program kwa uwazi na ufanisi.
Mafunzo hayo yametolewa katika vituo vya Utafiti wa Kilimo vilivyo chini ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), ambavyo ni Hombolo mkoani Dodoma; Tumbi mkoani Tabora; Kihinga mkoani Kigoma; Maruku mkoani Kagera; na Ukiriguru mkoani Mwanza.
Programu ya TFSRP inalenga kuhakikisha kuwa tafiti na uzalishaji wa mazao vinafanyika kwa kuzingatia misingi uendelevu ya uhifadhi wa mazingira, usalama wa afya mahala pa kazi, na ujumlishwaji wa maswala ya kijinsia. Hatua hii itachangia kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa wananchi.