Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

TIJA INAYOPATIKANA KATIKA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA TFSRP

Imewekwa: 16 Sep, 2025
TIJA INAYOPATIKANA KATIKA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA TFSRP

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli awahakikishia wadau wa Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula Tanzania (TFSRP) kuwa mipango na malengo ya Serikali iliyojipangia kupitia mradi huo yanaleta matokeo chanya kama yalivyokusudiwa.  Amesema hayo wakati akifungua Warsha ya siku tatu ya wadau wa programu ya TFSRP, tarehe 16 Septemba 2025, jijini Arusha.
 
Aidha, Katibu Mkuu Mweli amehamasisha wadau kutoa maoni na kueleza kuwa Wizara ya Kilimo ipo tayari kuyapokea ili kuzidi kuboresha utekelezaji wa programu hiyo muhimu yenye gharama zaidi ya Dola za Marekani milioni 300.  Ameeleza kuwa kwa sasa Serikali imeanza hatua za awali za kuwa na Maabara ya Kisasa ya Bio-Science.
 
“Naishukuru sana Benki ya Dunia kwa kutuamini na kuamua kusafiri na sisi katika kuleta mabadiliko kwenye Sekta ya Kilimo kwa Bara na Zanzibar.  Kwa upande wa Serikali tupo tayari kushirikiana na Sekta Binafsi na tutaendelea kuwa nao karibu kwa kutambua ni eneo lipi la kushirikiana nao ilikuleta mabadiliko yanayoleta tija kwa wakulima,” ameeleza Katibu Mkuu Mweli.  
 
Ameongeza pia kuna maeneo ambayo yanahitaji uwekezaji wenye tija husuan kwenye mafuta ya kula, zao la ngano (yaani import substitution crops - edible oil and wheat) na pia eneo la mikopo yenye riba kubwa (higher financial loan schemes).
 
Kuhusu maoni ya wadau katika kushirikiana (synergy), Katibu Mkuu Mweli ameeleza utayari wa Wizara ya Kilimo ipo tayari kuendelea kuboresha utekelezaji wa programu ya TFSRP kwa manufaa mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla. 
 
Programu ya TFSRP imehusisha usambazaji wa teknolojia zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi katika kilimo nchini ambapo takribani hekta 37,000 za ardhi zinatarajiwa kuwa na miundombinu ya umwagiliaji na uchimbaji wa visima kwa wakulima wadogo; usambazaji wa huduma za ugani kwa wakulima; upimaji wa afya ya udongo; uimarishaji wa tafiti za mbegu na pembejeo za kilimo ili kupunguza gharama za uzalishaji ambapo matokeo yanayotarajiwa ni kufikia wakulima takribani 300,000 ili watumie teknolojia za kuongeza ustahimilivu ambapo kati yao ni wakulima wanawake 120,000.