UPIMAJI WA AFYA YA UDONGO WABADILISHA KILIMO KYELA
Wakulima Wilayani Kyela wameishukuru Serikali kwa kuanzisha zoezi la upimaji wa afya ya udongo, wakieleza kuwa hatua hiyo itabadilisha mfumo wao wa kilimo na kuwasaidia kuzalisha kwa tija zaidi.
Akizungumza na wakulima hao, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Wakili Florah A. Luhala amesema kilimo ndicho chanzo kikuu cha mapato ya Halmashauri hiyo. Ameongeza kuwa elimu ya uhamasishaji inayotolewa itasaidia kuongeza hamasa kwa wakulima kutumia mbolea sahihi kwa wakati, jambo litakaloinua mapato na kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.
Katika ziara hiyo, baadhi ya wakulima waliokuwa sehemu ya upimaji wa udongo wamekabidhiwa vyeti vinavyoonesha afya ya udongo wa mashamba yao. Vyeti hivyo vitawarahisishia wakulima kufahamu ni aina gani ya mbolea inayofaa kwa mashamba yao, hivyo kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa kilimo.
Elimu hiyo imetolewa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Kilimo na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), huku wawakilishi wa Makampuni ya Mbolea wakitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu bidhaa wanazozalisha. Elimu hiyo imehusisha umuhimu wa kutumia pembejeo bora na za wakati ili kuongeza mavuno na kuboresha maisha ya wakulima.
Ziara ya uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea katika Nyanda za Juu Kusini inaratibiwa na Wizara ya Kilimo kwa lengo la kutoa elimu endelevu ya kanuni bora za kilimo, ikiwemo matumizi sahihi ya pembejeo, mbinu bora za kilimo na njia za kuongeza uzalishaji.