BENKI YA DUNIA, IFAD NA JICA WAKAGUA MAENDELEO YA TFSRP KWA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI
Ujumbe kutoka Benki ya Dunia (World Bank), Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (International Fund for Agricultural Development - IFAD) na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan - JICA) umefanya ziara ya kukagua utekelezaji (implementation support mission) wa Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) katika kituo cha utafiti wa kilimo cha TARI- Tengeru; TARI- Seliani na shamba la mbegu za kilimo la Ngaramtoni la Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), jijini Arusha tarehe 29 Septemba 2025.
Ujumbe ulitembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kupokelewa na Katibu Tawala Bw. Missaile Musa ambaye alishukuru wadau hao kwa kushirikiana na Serikali kuleta mageuzi yenye tija katika Sekta ya kilimo.
Wakiwa TARI - Tengeru, ujumbe ulipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana ambaye alieleza kuhusu tafiti zinazoendelea katika vituo mbalimbali vya TARI na kituo cha TARI-Tengeru kinachohusika na tafiti za mazao ya mbogamboga, matunda, viungo na vikolezo.
Alieleza kuhusu mbegu mpya za mbogamboga zilizofanyiwa utafiti chini ya programu ya TFSRP ambazo ni: pilipili kichaa (mbegu aina 5), pilipili hoho (mbegu aina 5), pilipilimbuzi (mbegu aina 3), na nyanya (mbegu aina 6). Aina hizi za mbegu zinauwezo wa kuhimili magonjwa, ikiwemo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na huzalishaji wa mazao mengi.
Ujumbe ulikagua pia miche mbalimbali ya tafiti ikiwemo migomba, parachichi, miche ya viungo; na ukaguzi wa maabara za utafiti (tissue culture).
Katika kituo cha TARI - Seliani, ujumbe ulikagua maabara ya tafiti za udongo, utunzaji wa mbegu mama, eneo la ujenzi wa benki ya mbegu (Gene Bank) litakalowezesha utunzaji wa aina zote za mbegu kwa muda mrefu (miaka 100 na zaidi) hivyo kuondoa tatizo la kupotea kwa aina mbalimbali za mbegu za mazao nchini.
Katika shamba la Ngaramtoni - ASA, ujumbe ulielezwa kuhusu uzalishaji wa mbegu zikiwemo ngano, mahindi na kukagua mitambo miwili ya kusafisha mbegu na kuziweka katika vifungashio. Aidha, ujumbe pia ulipokea ushuhuda kutoka kwa Afisa Ugani kutoka Halmashauri ya Meru aliyenufaika na mafunzo yaliyotolewa kwa Maafisa Ugani 1701 chini ya programu ya TFSRP kwa ajili ya kufundisha wakulima teknolojia himilivu za uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Ziara hiyo inaendelea mkoani Arusha tarehe 30 Septemba 2025 ambapo ujumbe huo unatarajiwa kukagua utekelezaji wa skimu ya umwagiliaji ya Mapama katika Wilaya ya Meru chini ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC).