UWEKEZAJI WA SERIKALI KUIMARISHA TASNIA YA ZAO LA MPUNGA
Wizara ya Kilimo imesema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika tasnia ya mpunga nchini yametokana na uwekezaji wa kimkakati uliotekelezwa na Serikali, hatua iliyochangia kuimarika kwa usalama wa chakula, kuongezeka kwa ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kitaifa wa Wadau wa Zao la Mpunga uliofanyika Machi 30, 2026 mkoani Morogoro, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Prof. Peter L. M. Msoffe, amesema nchi imeendelea kushuhudia mageuzi makubwa kwenye kilimo kutokana na uwekezaji wa kuimarisha tasnia ya zao la mpunga.
Prof. Msoffe amebainisha kuwa, “uzalishaji wa mchele umefikia tani milioni 2.6 katika mwaka 2024/2025, ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 1.2, hali iliyoiwezesha Tanzania kuwa na ziada ya tani milioni 1.4 na kuimarisha usalama wa chakula nchini.” Ongezeko hilo la uzalishaji, tani 298,715 za mchele zimeuzwa katika masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Kusini mwa Afrika (SADC), na kuingiza zaidi ya shilingi bilioni 333.5 za fedha za kigeni.
Naye Bi. Pendo Bigambo (Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mazao na Viwango), ambaye amemwakilishi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) amesema kuwa “kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo mwaka 2023 kumeimarisha usimamizi wa mnyororo wa thamani wa mazao, ikiwemo mpunga, na kuongeza uwazi katika biashara.”
Kwa upande wake Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la JICA nchini Tanzania, Bw. ARA Hitoshi ameeleza kuwa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Japan (kupitia JICA) umechangia maendeleo makubwa katika Sekta ya Kilimo kupitia miradi mbalimbali inayoendana na mkakati wa taifa wa maendeleo ya mpunga.
Mkutano huo una kaulimbiu, “Mkakati wa Kuendeleza Zao la Mpunga, Nyenzo Kufikia DIRA 2050” umewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta, akiwemo Mkurugenzi Msaidizi wa Uzalishaji wa Mazao kutoa Wizara ya Kilimo, Bi. Kissa Chawe. Wadau wengine ni pamoja na maafisa kilimo kutoka mikoa na halmashauri mbalimbali, wakulima, wanaushirika na wadau wa maendeleo.