VIJANA 151 WA BBT MLAZO/NDOGOWE WAPATIWA MAFUNZO YA MATUMIZI VIUATILIFU
Vijana 151 wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) wamepatiwa mafunzo ya matumizi sahihi na salama ya viuatilifu katika Shamba la Pamoja la Dkt. Samia Suluhu Hassan lililopo Mlazo/Ndogowe jijini Dodoma tarehe 29 Novemba 2025, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu wa kilimo 2025/2026. Mafunzo hayo yametekelezwa na Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano na Taasisi yake ya Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA).
Lengo la mafunzo ni kuwaongezea vijana ujuzi wa kitaalamu katika matumizi ya viuatilifu ili kulinda afya, kuongeza uzalishaji na kupunguza athari kwa mazingira.
Afisa Mazingira na Jamii wa Mradi wa BBT Project 1 kutoka Wizara ya Kilimo, Bi. Anna Moshi amebainisha kuwa matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu yamekuwa chanzo cha madhara kwa wakulima na ardhi, hivyo mafunzo endelevu kwa vijana wa BBT ni muhimu ili kuhakikisha matumizi yanazingatia viwango vilivyowekwa na mamlaka husika.
Mmoja wa wanufaika wa mafunzo, Bi. Regina Protas ameeleza kuwa elimu waliyoipata imewasaidia kutambua viuatilifu feki, kusoma maelekezo ya matumizi na kutekeleza hatua za usalama wakati wa kuteketeza mabaki ya dawa. Amesema uelewa huo utaboresha tija ya uzalishaji katika shamba la pamoja.
Naye Bi. Agnes Deus amesema kuwa mafunzo yamemwezesha kuelewa tofauti kati ya viuatilifu vya mguso na vya mfumo, jambo litakalorahisisha uchaguzi wa dawa kulingana na changamoto za mazao. Ameongeza kuwa ujuzi huo utawasaidia kuongeza mavuno katika msimu ujao.
Mafunzo yamehusisha mazoezi ya vitendo shambani, ambapo vijana wamefundishwa kupima, kuchanganya na kunyunyiza viuatilifu kwa usahihi, sambamba na matumizi ya vifaa kinga wakati wa kazi za kilimo. Washiriki wamesema mafunzo kwa vitendo yamewaongezea ujasiri wa kufanya shughuli hizo kwa kufuata taratibu za usalama.
Mafunzo yalianza tarehe 24 Novemba 2025 katika Shamba la Pamoja la BBT Chinangali kwa kufundisha jumla ya vijana 102 kwa siku nne na kuhitimishwa tarehe 29 Novemba 2025 kwa vijana wengine 151 waliofundishwa kwa siku nne katika shamba la Mlazo/Ndogowe, Dodoma.