Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

VIJANA WA BBT CHINANGALI WAPATIWA MAFUNZO YA VIUATILIFU

Imewekwa: 27 Nov, 2025
VIJANA WA BBT CHINANGALI WAPATIWA MAFUNZO YA VIUATILIFU

Vijana wanufaika wa Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) kupitia Mradi wa BBT Project I, wamepatiwa mafunzo ya matumizi sahihi na salama ya viuatilifu yaliyofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 26 Novemba 2025, katika Shamba la Chinangali lililopo mkoani Dodoma.

Mafunzo hayo yametolewa na Wataalamu kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kwa lengo la kuongeza uelewa na kanuni za usimamizi salama wa viuatilifu katika shughuli za kilimo, hususan katika kuendeleza kilimo endelevu.

Mafunzo hayo yamejikita katika kujenga uwezo wa vijana katika maeneo kadhaa muhimu ikiwemo matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga (PPE), taratibu za usalama kwa mtumiaji, mbinu za kitaalamu za kuchanganya na kunyunyizia viuatilifu, utambuzi wa viuatilifu vinavyokubalika kisheria, pamoja na kanuni za kulinda afya ya mimea, binadamu, na mazingira. 

Mafunzo yanalenga kuwajengea vijana umahiri wa vitendo wa kufanya maamuzi sahihi katika usimamizi wa viuatilifu ili kuongeza tija na kupunguza hatari za kiafya na kimazingira  kuelekea msimu wa kilimo 2025/2026. Hatua hiyo ni kuimarisha jitihada za Serikali katika kuongeza elimu na ujuzi wa kisasa ili vijana waongeze tija katika uzalishaji wa mazao.