WADAU WA KILIMO WAJENGEWA UWEZO KUTUMIA MASHINE ZA KUKAUSHA NA KUPIMA UNYEVU WA NAFAKA MKOANI MBEYA
Wadau wa Kilimo kutoka Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi wamepatiwa mafunzo juu ya matumizi ya mashine za kisasa za kukaushia na kupima unyevu wa mazao ya nafaka, katika warsha iliyoandaliwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) jijini Mbeya.
Warsha hiyo imefanyika tarehe 26 Novemba 2025 katika shamba la Raphael Group Ltd, ambapo mashine ya Batch Circulating Dryer iliyofungwa katika shamba hilo imewasilishwa kwa vitendo. Mashine hiyo ina uwezo wa kukaushia hadi tani nane za mpunga ndani ya saa nne, ikiwa ni teknolojia muhimu kwa kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mhandisi Sekela Mwakihaba, mwakilishi wa Katibu Mkuu kutoka Idara ya Zana za Kilimo na Uongezaji Thamani, amesema ushiriki wa wadau ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao ya nafaka na kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa nafaka kipindi cha uvunaji.
Ameeleza kuwa serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa kupitia utekelezaji wa Agenda 10/30, ikilenga kuongeza tija na thamani ya mazao ya kilimo ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza kipato kwa wakulima.
Kwa upande wake, Bw. Maisha Ambangile, Meneja wa Uzalishaji wa Raphael Group Ltd Kituo cha Uyole, amesema mashine hiyo itawasaidia wakulima kupunguza gharama na kuongeza ufanisi kwa kupata nafaka kavu ndani ya muda mfupi na kwa ubora unaotakiwa sokoni. Aidha, alibainisha kuwa mashine moja ya kukaushia nafaka inagharimu takribani shilingi milioni 188.
Warsha hiyo iliratibiwa na JICA kwa kushirikiana na kampuni za YAMAMOTO (watengenezaji wa mashine za kukaushia nafaka, pamoja na Kett Electric Laboratory, ambao ni watengenezaji wa mashine za kupima unyevu wa nafaka. Washiriki ni maafisa wa Serikali, wataalamu wa JICA, wamiliki wa Mtambo ya kukaushia nafaka, pamoja na wakulima kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya.