WADAU WA TANRICE3 WAKUTANA KUJADILI TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MRADI
Wadau wanaotekeleza Mradi wa (TANRICE3) wamekutana katika kikao cha sita kujadili taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kutoka kwa wadau pamoja na Vyuo 6 vya Mafunzo ya Kilimo (MATI) vya Ilonga; Mtwara; Igurusi; Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Kilimanjaro (KATC); Tumbi; Ukiriguru pamoja na Shule ya Kilimo Zanzibar, kwa lengo la kuwezesha ushiriki wa kutosha katika kutekeleza mradi huo.
Kikao hicho kimefanyika tarehe 13 Mei 2026 mkoani Kilimanjaro, na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka Wizara ya Kilimo; Wakala wa Taifa wa Mbegu za Kilimo (ASA); Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC); Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI); Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI); Wakufunzi kutoka Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo (MATI); Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar; Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar na wawakilishi kutoka Serikali za Mitaa.
Taarifa zimejikita katika maendeleo ya uzalishaji wa mbegu; zana za kilimo; usimamizi wa miradi ya umwagiliaji; jinsia; masoko; maendeleo ya utekelezaji wa Mfumo wa Taifa wa Tathmini ya Miundombinu ya Umwagiliaji (kwa kutumia mfumo mpya wa kidijiti utakaotumika kusimamia na kutunza kumbukumbu za taarifa za mafunzo ya kilimo cha mpunga nchini (NaRDA)), katika kuwezesha utoaji wa msaada wa kiufundi kwa wakulima wa mpunga ili kufanikisha mafunzo hayo kulingana na hali ya skimu husika.
Mshauri Elekezi wa Mradi wa TANRICE3, Bw. Takanori Tomizuka ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutenga shilingi milioni 67 kwa ajili ya mafunzo kwa wakulima wa mpunga, hatua inayoongeza upatikanaji wa elimu sahihi ya kilimo cha mpunga na kuongeza uzalishaji.
Bw. Tomizuka pia ametoa pongezi kwa Vyuo vya Kilimo nchini kwa kuweka kipaumbele katika suala zima la mafunzo kwa wakulima. Aidha, amekipongeza chuo cha MATI- Igurusi kilichoweza kutenga fedha na muda kwa ajili ya mafunzo ya kuboresha utendaji (uboreshaji endelevu) "Kaizen" huku akihamasisha vyuo vingine kufanya hivyo.
Mradi wa TANRICE3 unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan ( JICA) kwa jumla ya Dola za Marekani 6,102,085. Mradi umejikita katika kukuza tasnia ya zao la mpunga nchini kwa kuwajengea uwezo wakulima kupitia mafunzo ambapo hadi sasa jumla ya wakulima 6116 (wanaume 3291 na wanawake 2825 ) wamenufaika na mafunzo hayo, hatua iliyoongeza uzalishaji wa kutoka tani 3.25 kwa hekta hadi kufikia tani 4.63 kwa hekta sawa na ongezeka la 40%.