Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WAKULIMA 202 WANUFAIKA NA HUDUMA YA UMWAGILIAJI MKOANI GEITA

Imewekwa: 28 Oct, 2025
WAKULIMA 202 WANUFAIKA NA HUDUMA YA UMWAGILIAJI MKOANI GEITA

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imezindua na kukabidhi vifaa vya kisasa vya umwagiliaji kwa wakulima 202 katika Mkoa wa Geita, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuinua Sekta ya Kilimo na kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji bila kutegemea mvua pekee.

Uzinduzi huo umefanyika tarehe 27 Oktoba 2025 katika Kijiji cha Buzirayombo, Kata ya Bukome, Wilaya ya Chato, ambapo vifaa hivyo vimekabidhiwa rasmi kwa wakulima watakaonufaika na huduma hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe. Louis Bura ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali wakulima kupitia uwezeshaji wa vifaa vya umwagiliaji, akibainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kupunguza umasikini, kukuza uzalishaji, na kuboresha kipato cha wananchi kupitia Sekta ya Kilimo.

Mhe. Bura ameeleza kuwa katika awamu ya kwanza, jumla ya jozi 20 za pampu za umwagiliaji zimetolewa kwa wakulima, na akatoa rai kwa wanufaika wote kuhudhuria mafunzo maalum kuhusu matumizi sahihi ya vifaa hivyo, ili kuhakikisha vinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya katika uzalishaji.

Kwa upande wake, Mratibu wa Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula Nchini (TFSRP),  Bw. Timothy Semuguruka, amesema kuwa programu hiyo inalenga kubadilisha mfumo wa kilimo kutoka kutegemea mvua pekee hadi kutumia mbinu endelevu za umwagiliaji. Ameongeza kuwa utekelezaji wake unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, sambamba na kupunguza utegemezi wa misimu ya mvua.

Vifaa hivyo vitaimarisha mahitaji ya wakulima mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata kipato endelevu na chakula cha kutosha kupitia matumizi bora ya teknolojia za kisasa za umwagiliaji.