WAKULIMA KUFAIDIKA NA MAJARIBIO YA KUPIMA UDONGO KUPUNGUZA TINDAKILI
Wizara ya Kilimo imeanza majaribio ya kupima udongo kukabiliana na tindikali katika Mikoa ya Njombe, Iringa na Katavi tarehe 30 Septemba 2025. Walengwa ni wakulima wadogo ili wapatiwe elimu za kukabiliana na athari za tindikali kwenye udongo ikiwa pamoja na kuwafundisha namna ya matumizi ya mbolea asilia (organical mineral) pamoka na chokaa mzao ili kupunguza wingi wa tindikali mashambani.
Timu ya wataalamu kutoka Idara ya Usimamizi na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kilimo imefanya zoezi la kuchukua majira ya nukta na kupima pH katika mashamba ya wakulima 22,000 katika mikoa hiyo. Zoezi hilo ni la miaka 3 kuanzia kipindi cha 2025/2026 kupitia Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) kwa kufanikisha kiashiria kidogo namba 7.2 (DLI 7.2) kinachohusu majaribio ya mbolea na visaidizi vya mbolea kwa ajili ya kupunguza tindikali kwenye udongo,.
Wataalam pia wametoa elimu kwa baadhi ya wakulima wa maeneo hayo pamoja na kukubaliana kutenga maeneo maalumu yatakayotumika kama mashamba darasa yatakayosimamiwa na wakulima husika na Wizara itawawezesha pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu, mbolea na chokaa mazao ili mashamba hayo yatumike kufundishia wengine.
Mhandisi Juma Mdeke, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mipango Bora ya Ardhi ya Kilimo amesema kwa sasa wanafanya majaribio hayo kwa wakulima baada ya kuwapatia mafunzo maalumu juu ya athari ya wingi wa tindikali katika ardhi za kilimo na namna ya kuweza kupunguza athari hizo na kuongeza tija ya mazao.
“Ukanda huu wa Nyanda ya Juu Kusini Njombe, Iringa pamoja na Mkoa wa Katavi hususan kwenye baadhi ya Wilaya kumeathirika zaidi na tindikali. Zoezi letu ni la kimkakati ili kupunguza ukali huo na tutawaelekeza wakulima wetu kutumia mbolea kama dawa ya kutokomeza kabisa tindikali ili waweze kunufaika na tija kwenye mazao wanayozalisha,” amesema Mhandisi Mdeke.