Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WAKULIMA WA PAMBA KUKAA MGUU SAWA, PAMBA FURSA KIUCHUMI

Imewekwa: 16 Jun, 2025
WAKULIMA WA PAMBA KUKAA MGUU SAWA, PAMBA FURSA KIUCHUMI

Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua viwanda viwili  cha Pamba na Mabomba mkoani Simiyu huku akisisitiza kuwa,  Serikali imedhamiria kufanya uwekezaji katika zao hilo na mabadiliko yake yataonekana taratibu kwa kukuza uchumi wa nchi, mkoa na watu.

Amesema hayo katika ziara yake Mkoani Simiyu wakati akizindua viwanda hivyo viwili ambavyo ni kiwanda cha kuchakata mabomba pamoja na kiwanda cha kuchakata pamba, katika eneo la Salunda, wilayani Bariadi. 

“Nawashukuru wananchi kwa mapokezi.
Nimefungua kiwanda hiki cha mabomba na kuchakata pamba, nimeona kazi inayofanywa na ubora wake nimejiridhisha, hatua hii itapunguza matumizi ya fedha za kigeni katika zao la pamba,” amesema Mhe. Rais Dkt. Samia.

Amesisitiza kuwa, kama ambavyo nchi imefanya vizuri katika zao la korosho, kahawa, tumbaku, mbaazi ndivyo ambavyo kwa sasa Serikali inaenda kuweka nguvu katika kulipandisha zao la pamba.

“Tukiwa na wazee jana jioni Waziri wa Kilimo alitueleza mengi mipango ya Serikali katika kuliwezesha zao hili la pamba, tumepandisha zao moja moja sasa tumegeukia pamba hatua tunazochukua ni kwa faida yetu, mabadiliko yanakuwa na maumivu kidogo watakaoumia ni wale ambao hawalimi wanaonunua mazao kwa kuwalalia wakulima na hao ndio wanakuwa na kelele,” amesema Mhe. Rais Dkt. Samia.

Ameongeza kuwa, mwekezaji wa kiwanda hicho amewaza vyema na ataungana na Serikali kuhakikisha nchi inasitisha upelekaji malighafi za pamba na kuitengeneza hapa hapa nchini ili watu wapate ajira.

Viwanda hivyo vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 8, vinamilikiwa na Kampuni ya Moli Oil Mills Company Ltd., ambao pia ni wamiliki wa kampuni za Nsagali. 

Aidha, viwanda hivyo vimezalisha takribani ajira 850 za moja kwa moja, pamoja na ajira nyingine 400, huku vikitoa fursa kwa wajasiriamali wadogo wadogo kunufaika kwa kufanya biashara za mama lishe. 

Mhe. Rais Dkt. Samia yuko katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu, hadi Juni 19, 2025.