Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WAKULIMA WAHIMIZWA AFYA YA UDONGO NDIYO NGUZO YA UZALISHAJI BORA

Imewekwa: 18 Oct, 2025
WAKULIMA WAHIMIZWA AFYA YA UDONGO NDIYO NGUZO YA UZALISHAJI BORA

Wakulima wapatiwa wito kuwa upimaji wa afya ya udongo ni moja ya nguzo ya kuongeza uzalishaji na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.

Wito huo umetolewa tarehe 16 Oktoba 2025 katika Kijiji cha Utende, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, wakati wa kampeni ya “Mali Shambani: Silaha Mbolea” inayolenga kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea, usajili wa wakulima kwenye mpango wa ruzuku na upimaji wa afya ya udongo.

Afisa Kilimo wa Mkoa wa Katavi, Bw.Faridu Abdallah amefafanua kuwa na udongo wenye afya ni msingi wa kilimo endelevu na mavuno bora huku akisisitiza wakulima watumie matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija na ubora wa mazao.  Aidha, ametoa angalizo kuwa matumizi mabaya ya mbolea na mbinu zisizo rafiki kwa mazingira hudhoofisha rutuba.

Mkulima Bw. Daudi Palazi amechangia kuwa upimaji wa afya ya udongo katika shamba lake umemsaidia kujua virutubishi vinavyohitajika shambani na kupunguza gharama za uzalishaji huku mavuno yakiongezeka.

Katika nyakati tofauti ya mkutano na wakulima wa kijiji cha Tumaini kilichopo Halmashauri ya Nsimbo, mkoani Katavi, Bw. Samson Poneja, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Maendeleo ya Mazao iliyopo Wizara ya Kilimo amekabidhi vyeti kwa wakulima waliopima afya ya udongo na kupongeza hatua hiyo kama mfano wa kuigwa.

Wizara ya Kilimo inaendelea na ziara nyingine ya kuzunguka Mikoa mbalimbali kupima afya ya udongo ikiwemo Njombe, Iringa, Mbeya, Shinyanga, Mwanza, Songwe na Katavi ambapo wakulima wanahamasishwa kuendelea kupokea huduma za kupimiwa afya ya udongo, kutumia mbolea kwa usahihi na kusajili mashamba yao ili kuongeza tija na uzalishaji.