Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WAKULIMA ZAIDI YA 150 WA WILAYA YA IKUNGI WAPATIWA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA NCHINI

Imewekwa: 06 Dec, 2025
WAKULIMA ZAIDI YA 150 WA WILAYA YA IKUNGI WAPATIWA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA NCHINI

Wakulima zaidi ya 150 katika Wilaya ya Ikungi, Mkoa wa Singida wapatiwa mafunzo ya matumizi sahihi ya mbolea ikiwa ni utekelezaji wa kampeni ya Wizara ya Kilimo ya “Mali Shambani, Silaha Mbolea” iliyoanza mkoani humo tarehe 03 Desemba 2025. 

Kampeni hiyo itahusisha pia mikoa ya Tabora, Kigoma, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mara, Mwanza na Kagera ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao nchini.  Mikoa minginie ambayo tayari elimu imetolewa wakati wa awamu ya awali ni Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya, Rukwa, Songwe na Katavi. 

Mafunzo hayo yanaongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao, Bw. Samson Poneja, pamoja na Afisa Kilimo Mkuu Mwandamizi, Bw. Alphonce Mwiru, wakishirikiana na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za Wizara ikiwemo Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), pamoja na makampuni ya usambazaji na uuzaji wa pembejeo kutoka kanda ya kati.

Kwa mujibu wa Bw. Mwiru, pamoja na kwamba matumizi ya mbolea yameongezeka kwa wakulima wengi, bado kuna changamoto ya uelewa sahihi wa jinsi ya kutumia mbolea kwa kiwango, aina na muda sahihi.

“Wakulima wengi wamehamasika kutumia mbolea lakini hawana elimu sahihi ya matumizi ya mbolea hizo kwa namna moja ama nyingine.  Ni jukumu letu kutoka maofisini hasa kipindi hiki cha msimu wa kilimo ili kutatua kitaalamu changamoto zozote,” amesema Bw. Mwiru

Kampeni inahusisha pia usajili wa wakulima katika mfumo wa kidijiti na upimaji wa afya ya udongo katika mashamba ili kutoa ushauri wa kitaalamu, kubaini mahitaji halisi ya wakulima, na kupanga mikakati stahiki ya kuongeza upatikanaji wa mbolea na huduma nyingine za kilimo katika mikoa husika.

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekuwa na mikakati kabambe ya kutaka kumkomboa mkulima kwa kuimarisha huduma za ugani, kuanzisha vituo vya zana za kilimo, kuongeza maghala na masoko ya mazao, kujenga na kukarabati miundombinu ya umwagiliaji, kuwezesha upatikanaji wa mbegu za ruzuku na pembejeo za kilimo.  Lengo la Serikali ni kukuza kilimo kwa asilimia 10 hadi ifikapo mwaka 2030.