Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WANAHABARI WAHAMASISHWA KURIPOTI MAGEUZI KATIKA SEKTA YA KILIMO

Imewekwa: 31 Mar, 2026
WANAHABARI WAHAMASISHWA KURIPOTI MAGEUZI KATIKA SEKTA YA KILIMO

Wanahabari wametakiwa kuhabarisha Umma mageuzi makubwa yanayofanywa na Serikali katika Sekta ya Kilimo ili wananchI wanufaike na fursa zinazopatika katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta hiyo.

Ametoa wito huo Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Zana za Kilimo na Umwagiliaji, Mha. Athumani Kilundumya alipokutana na wawakilishi wa magazeti ya “The Guardian na Nipashe”; na  Kampuni ya Magazeti ya Serikali - TSN inayoendesha “Daily News na Habari Leo”.

Mazungumzo hayo yamefanyika tarehe 27 Machi 2026 katika moja ya kumbi ndogo za Wizara ya Kilimo zilizopo Mtumba, jijini Dodoma, ambapo Naibu Katibu Mkuu Mha. Kilundumya amewashukuru wawakilishi hao kwa ushirikiano na kuwataka kuimarisha kazi zao katika mitandao ya kijamii kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli za Serikali katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo ili kuepuka mitazamo hası ambayo haina tija katika kujenga Taifa.  

Aidha, Mha. Kilundumya ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, Awamu ya Pili chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha Sekta ya Kilimo, ikiwemo ununuzi wa vifaa vya uchimbaji visima na uanzishwaji wa vituo vya zana za kilimo, hatua inayolenga kuongeza tija na upatikanaji wa huduma kwa wakulima nchini.

Kwa upande wake, Mhariri Mtendaji wa gazeti la The Guardian / Nipashe, Bi. Salome Kitomari ameishukuru Wizara kwa ushirikiano unaoendelea na kuahidi kuudumisha kwa manufaa ya pande zote.

Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Bi. Soter Salema, ameeleza kuwa  TSN ipo tayari kukuza ushirikiano kwa kuitangaza Sekta ya Kilimo na mafanikio yake kwa Umma ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Wizara katika maeneo mengine yenye kuleta tija kwa wakulima na wananchi kwa ujumla