WATAALAMU WA AFYA YA UDONGO WATAKIWA KUWA NA TIMU BORA, KUFANYA KAZI KWA UFANISI
Wataalamu wanaohusika na zoezi la ukusanyaji wa sampuli za udongo kwa ajili ya upimaji wa afya ya udongo nchini, wamefanya kikao kazi kinacholenga kujadili na kutoa elimu ya namna bora ya ukusanyaji wa sampuli za udongo, kwa ajili ya upatikanaji wa ramani ya afya ya udongo kidigitali pamoja na usimamizi sahihi wa ardhi ya kilimo.
Kikao kazi hicho kimefanyika tarehe 6 Januari 2026 mkoani Morogoro na kuhusisha wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo; Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI); Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB); Bodi ya Mkonge Tanzania; Chuo cha Sukari cha Taifa; Vyuo vya Kilimo ( MATI); maafisa kilimo; wataalamu kutoka Chuo cha Kilimo cha Sokoine ( SUA); Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA); pamoja na wahitimu kutoka katika vyuo mbalimbali nchini.
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Mha. Juma Mdeke, amewataka washiriki wa zoezi hilo kuhakikisha wanajenga timu imara kwa kuzingatia misingi ya mawasiliano bora, uhusiano wa karibu, kujiamini pamoja na kuwa tayari kutoa na kupokea mrejesho.
Naye Afisa Kilimo Mkuu na Afisa Kiungo wa Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) katika kiashiria namba 7, Bw. Ntirankiza Misibo amesema zoezi hili litawezesha upatikanaji wa ramani ya afya ya udongo kidigitali, itakayotoa taarifa sahihi kuhusu aina ya udongo, zao linalostahili kulimwa katika udongo huo, matumizi sahihi ya mbolea pamoja na matumizi sahihi ya zana za kilimo.
Hatua hii ni utekelezaji wa Mikakati ya Wizara ya Kilimo kupitia Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) kiashiria namba 7, zoezi ambalo ni uhaulishaji wa upimaji wa afya ya udongo wa mwaka 1984 uliofanyika kwa mizani ya 1:2000000, upimaji wa sasa unafanyika kwa mizani ya 1:50000 ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa za kina nchini kuhusu afya ya udongo.
Jumla ya mikoa 13 nchini imefikiwa na zoezi la upimaji wa afya ya udongo na hivi sasa wataalamu wanaendelea na ukusanyaji wa sampuli za udongo katika mikoa ya Tabora, Morogoro, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara.