Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WAZIRI BASHE AKABIDHI MAGARI 38 YENYE THAMANI YA BILIONI 4.2

Imewekwa: 14 May, 2025
WAZIRI BASHE AKABIDHI MAGARI 38 YENYE THAMANI YA BILIONI 4.2

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amekabidhi Magari 38 yenye thamani ya shilingi Bilioni 4.2 kwa ajili ya kusimamia na kutekeleza majukumu ya Sekta ya Kilimo; pamoja na magari 7 ya mitambo ya  Uchimbaji Visima tarehe 12 Mei 2025, jijini Dodoma. 

Magari hayo yamekabidhiwa kama ifuatavyo: Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) magari (14) kwa ajili ya kusimamia na kudhibiti utoroshaji wa mazao mipakani; Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) magari (5) kusimamia Vyama vya Ushirika na Vyama vya Msingi; Bodi ya Mkonge Tanzania magari (2) kwa ajili ya kuendesha shughuli za Tasnia ya Mkonge, lengo ikiwa ni kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo kupitia Agenda 10/30.

Aidha, mitambo (7) ya Uchimbaji Visima yamekabidhiwa kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kwa ajili ya uchimbaji wa visima kwa wakulima hususan Wakulima wadogo, mitambo hiyo ina uwezo wa kuchimba visima hadi mita 300 na mitambo  mingine inauwezo wa kuchimba visima  hadi mita 1800;

Hatua hii inaenda sambamba na lengo la Serikali katika utoaji wa ruzuku kwa wakulima, ambapo ukiachana na ruzuku ya mbegu na mbolea pia imelenga kutoa ruzuku ya uchimbaji wa visima pamoja na huduma za zana za kilimo kwa wakulima 

Sambamba na hilo Mhe. Bashe pia amekabidhi magari (20) kwa Wizara ya Kilimo kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya kiutendaji kwa ufanisi zaidi.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb); Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli; Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Hussein Mohamed Omar; Makamu Mwenyeketi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mariam Ditopile (Mb); Menejimenti ya Wizara; na Watumishi wa Wizara, Taasisi/Bodi za Wizara ya Kilimo.