WAZIRI CHONGOLO AIFAGILIA TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI KWA SKIMU YA NDANDA
Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) ameipongeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kwa ujenzi wa skimu ya umwagiliaji ya Ndanda itakayonufaisha wakulima takribani 700 kutoka vijiji 7 vilivyopo ndani ya Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Amesema hayo tarehe 12 Desemba 2025 wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa mradi huo wenye hekta 350 na gharama zaidi ya Shilingi Bilioni 20. Mradi huo pia utahusisha ujenzi wa bwawa lenye kina cha mita 8 na urefu wa mita 960 litakaloweza kuvuna mita za ujazo milioni 3.6 za maji; ujenzi wa utoro wa maji (spillway) yenye urefu wa mita 523 na upana wa mita 40; mifereji mikuu 2 ya kilomita 9.5; mifereji ya kati ya kilomita 6.6 na mifereji midogo ya kilomita 17.2.
Katika hatua nyingine, Waziri Chongolo amepanda mti wa mchungwa kwenye Ofisi ya Umwagiliaji ya Wilaya ya Masasi, ambao ni ujenzi unaotokana na mradi huo wa skimu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba ya meneja wa mradi na ujenzi wa maabara ya kupima ubora wa vifaa vya ujenzi na udongo unaotumika.
Akizungumza na wanavijiji kutoka vijiji vya Mwena, Mwena A, Chibwini, Mpohola na Njenga katika Wilaya ya Masasi; na pia vijiji vya Likwachu na Nandanga katika Wilaya ya Ruangwa, Waziri Chongolo amewahakikishia kuwa elimu kuhusu mradi huo ni endelevu ambapo wataalamu wa ujenzi, kilimo, umwagiliaji na mazingira wataendelea kutoa elimu kuhusu mradi huo na matarajio yake hususan katika kilimo na mabadiliko ya tabianchi.
“Bwawa litakalowekwa ata ufugaji wa samaki utawezekana ili wakulima wanufaike kikamilifu na miundombinu ya mradi, huku watakuwa wakilima na kuvuna mazao kwa uhakika wa upatikanaji wa maji kwa misimu mitatu hadi minne kwa mwaka pasipo kutegemea mvua,” ameeleza Waziri Chongolo. Mradi huo pia unatarajiwa kuongeza mavuno ya mazao kutoka wastani wa gunia 13 kwa ekari hadi kufikia gunia 35 kwa ekari.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Bw. Raymond Mndolwa ameleza kuwa mradi huo utatoa ajira kwa vijana katika shughuli za kilimo biashara, hususan katika mazao yanayotumia muda mfupi. Ameongeza pia NIRC Itatekeleza maelekezo yaliyotolewa ya kusimamia mradi huo ili mkandarasi akamilishe kwa muda unaotarajiwa ili wakulima waanze kunufaika ipasavyo.
Skimu ya Ndanda ni moja ya skimu 26 za umwagiliaji zilizopo katika upande wa Mkoa wa Mtwara na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2026.