WAZIRI CHONGOLO APONGEZA UKUAJI WA KASI YA COOP BANK; NA KUTOA MAJAWABU YA MITAJI KWA WANAUSHIRIKA
Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Godfrey Chongolo (Mb) ameipongeza Benki ya Ushirika Tanzania (Coop Bank Tanzania) kwa kukuza kiwango cha fedha katika kitabu cha mikopo kutoka Shilingi Bilioni 15 mwezi Januari 2025 hadi sasa kufikia Shilingi Bilioni 52, sawa na ukuaji wa asilimia 245; huku amana (deposit) ikiongezeka kutoka Shilingi Bilioni 19 hadi Shilingi Bilioni 60, sawa na asilimia 216 ya ukuaji.
Benki hiyo pia imekuza mizania (balance sheet) yake kutoka Shilingi Bilioni 49 mwezi Januari 2025 hadi sasa kufikia Shilingi Bilioni 114, sawa na ukuaji wa asilimia 133.
Ametoa pongezi hizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Bank Tanzania, Bw. Godfrey Ng’urah wakati wa mazungumzo yao kwenye Ofisi yake tarehe 20 Novemba 2025, jijini Dodoma; kufuatia hatua ya Benki hiyo kuendelea kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Uzinduzi wa Benki tarehe 28 Aprili 2025, Dodoma.
“Ushirika ni kama nyumba yenye msingi imara katika kusaidia Wakulima. Na ushirika wetu ni wa kilimo kuanzia maandalizi ya shamba hadi kupata matokeo. Hivyo, jambo la msingi ni Benki ya Coop kuimarisha huduma za kifedha na Wanaushirika ndani yake ili kufikia malengo yenye tija,” amesema Mhe. Waziri Chongolo.
Mhe. Waziri Chongolo ameahidi kuendeleza ushirikiano na Benki hiyo, huku akiwataka Watendaji wa Benki ya Coop kuongeza ubunifu zaidi katika utoaji huduma.
“Ningetamani kuona katika biashara yoyote inayohusu kilimo basi Benki ya Ushirika inakuwa mnufaika wa kwanza (beneficiary),” amesema Mhe. Waziri Chongolo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Benki ya Coop Tanzania, Bw. Ng’urah amesema kuwa Benki yake imeendelea kutekeleza dhamira ya kuchagiza uchumi jumuishi kwa kutoa huduma za kifedha, uwezeshaji wa kujenga maghala na masoko. “Tuna matawi 4 kwa sasa katika mikoa ya Dodoma, Kilimanjaro, Mtwara na Tabora. Malengo ya Benki ni kuongeza matawi mengine 4 mwisho wa mwaka katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera, Mwanza na Songwe,” amesema Bw. Ng’urah.