WAZIRI CHONGOLO AWATANGAZIA WAKULIMA WA IDOFI NEEMA YA MRADI WA UMWAGILIAJI
Wakulima wa Idofi, Wilaya ya Makambako wameishukuru Serikali kufuatia kusogezewa mradi mkubwa wa umwagiliaji unaotekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NiRC) utakaonufaisha ekari zaidi ya 1.300. Kwa mujibu wa tathmini ya awali ya wataalamu, mradi huo utahusisha ujenzi wa bwawa la umwagiliaji na uwekaji wa miundombinu ya kisasa itakayowezesha uzalishaji wa mazao mwaka mzima.
Wamesema hayo wakati wa mkutano wa hadhara wa Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) katika viwanja vya shule ya Msingi ya Idofi ambapo amewalekeza kuwa mradi huo wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu ya Idofi, utawezesha kilimo chenye tija na kufungua fursa mbalimbali za maendeleo katika eneo hilo.
Waziri Chongolo amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza fedha nyingi katika miradi ya kilimo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanatumia kikamilifu rasilimali zilizopo ili kujiletea maendeleo endelevu.
“Wataalamu wamebaini kuwa eneo linalolimwa kwa sasa halifiki ekari 300, wakati eneo lote lina ukubwa wa ekari 1,300. Eneo Hilo likiboreshwa, wananchi wataweza kulima eneo lote kwa tija na kuinua uchumi hii ni fursa kwetu wananchi wa Makambako,” amesema Waziri Chongolo.
Aidha, amewahakikishia wananchi kuwa hakuna mkulima atakayepoteza eneo lake kutokana na utekelezaji wa mradi huo; isipokuwa yule atayehama kwa hiari au kuuza eneo lake.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Makambako, Bw. Kenneth Haule, amewahimiza wananchi kujifunza kutoka katika maeneo ambayo tayari yamenufaika na miradi ya umwagiliaji kama vile Igomelo, Pawaga na Itipingi, ambako uzalishaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Usanifu Mha. Sadati Kolowa kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji amebainisha kuwa ushirikishwaji wa wananchi ni kipaumbele katika miradi yote ya umwagiliaji, kuanzia hatua za awali hadi utekelezaji wake, ili kuhakikisha kunakuwa na uelewa na maridhiano ya pamoja.