Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WAZIRI MKUU AWAKUMBUSHA WANANCHI KULA MLO SAHIHI

Imewekwa: 16 Oct, 2025
WAZIRI MKUU AWAKUMBUSHA WANANCHI KULA MLO SAHIHI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amewataka wananchi kuzingatia utaratibu wa kula mlo sahihi ili kujiepusha na ulaji usio sahihi ambao  ni  chanzo cha unene wa kupitiliza ambao kwa sasa umekuwa changamoto kwa jamii.

Ameeleza kuwa hali udumavu na ukondefu kwa watoto chini ya miaka mitano kwa kiasi umepungua.  Changamoto iliyopo ni unene uliozidi miongoni mwa wanawake na wanaume.  Amewataka wananchi kuzingatia ulaji wa milo sahihi na kufanya mazoezi ili kuondoa mwilini chakula kisichohitajika ili kujiepusha na changamoto ya magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kama kisukari na shinikizo la damu. 

Mhe. Waziri Mkuu ametoa hotuba yake ya kufunga Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani tarehe 16 Oktoba 2025, katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, Mkoani Tanga.  Amehimiza jamii kuongeza jitihada za uzalishaji chakula jambo ambalo ni msingi wa usalama wa chakula nchini hii ni sambamba na uhifadhi, na usindikaji wa chakula ili kuongeza tija kwa wakulima.

Ameelekeza viongozi wa Taasisi zote za kiserikali dini na zisizo za kiserikali kushirikiana na Serikali kuhamasisha matumizi ya teknolojia bora za kilimo ili kuboresha uzalishaji katika kilimo.

Mhe. Waziri Mkuu amezitaka Halmashauri zote kutenga bajeti za lishe na kuhakikisha elimu ya lishe inatolewa kwa kijamii.  Pili,  watalaam wa kilimo kutoka elimu juu ya mbinu bora za uzalishaji, uongezaji thamani wa mazao baada ya kuvunwa na uhifadhi wa chakula ili kuwa na chakula cha kutosha; sambamba na utunzaji mazingira.

Amemalizia hotuba yake kwa kuwakumbusha  wananchi kilimo ni mkombozi wa Chakula na ajira; huku akiwataka wakulima kuzitumia mvua za vuli zinazoendelea kunyesha hapa nchini Kwa ajili ya shughuli za kilimo ili kujenga Taifa lenye watu wenye afya bora.

Maadhimisho yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, Wakuu wa Mikoa ya Morogoro, Manyara, Kilimanjaro na Arusha; Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Stephen Nindi; Wawakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN), FAO, pamoja na Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri.