WAZIRI MKUU AZINDUA ACSAM
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), amesema Tanzania inachukulia matumizi endelevu ya zana za kilimo kama hitaji la kimkakati katika kuleta mageuzi ya Sekta ya Kilimo, kuongeza uzalishaji na kujenga mifumo himilivu ya chakula Barani Afrika.
Amesema hayo wakati akifungua rasmi Mkutano wa Kwanza wa Kikanda wa Afrika kuhusu Matumizi Endelevu ya Zana za Kilimo (Africa Conference on Sustainable Agricultural Mechanization – ACSAM) unaofanyika jijini Dar es Salaam kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
Mhe. Mwigulu ameeleza jitihada za Bara la Afrika kupitia Mfumo wa Zana Endelevu za Kilimo Barani Afrika (F-SAMA), Azimio la CAADP Kampala pamoja na Mkakati wa Miaka 10 wa CAADP (2026–2035) zinaonesha dhamira ya pamoja ya kuimarisha uzalishaji wa chakula, kuongeza uwekezaji, kujenga mifumo himilivu na kuhakikisha usalama wa chakula na lishe.
Katika kutekeleza ajenda hiyo, Waziri Mkuu amesema Tanzania imeongeza uwekezaji katika huduma za zana za kilimo, uendelezaji wa ujuzi kwa vijana na kuimarisha taasisi za utafiti, ikiwemo kuandaa Mkakati wa Taifa wa Zana za Kilimo kwa kushirikiana na FAO, unaolenga kuimarisha matumizi na usimamizi endelevu wa teknolojia za kisasa katika mnyororo wa uzalishaji na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo.
Amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuanzisha vituo jumuishi vya huduma za zana za kilimo nchi nzima, ambapo itanunua matrekta elfu kumi (10,000) na zana zake kwa ajili ya kuanzisha vituo elfu moja (1,000) katika ngazi ya kata, hatua itakayoongeza tija, kupunguza gharama za uzalishaji na kuwawezesha wakulima kushiriki zaidi katika shughuli nyingine za kiuchumi.
Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, Sekta Binafsi, Taasisi za Utafiti na Washirika wa Maendeleo, akitangaza kuwa Serikali ya Tanzania iko tayari kushirikiana na FAO katika mpango wa kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Zana za Kilimo Barani Afrika, kabla ya kufungua rasmi mkutano huo na kuzindua Mkakati wa Taifa wa Zana za Kilimo Awamu ya Pili (2026–2035).