Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WAZIRI MKUU MGENI RASMI MKUTANO WA ACSAM

Imewekwa: 30 Jan, 2026
WAZIRI MKUU MGENI RASMI MKUTANO WA ACSAM

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa Afrika wa Matumizi Endelevu ya Zana za Kilimo (Africa Conference on Sustainable Agricultural Mechanization – ACSAM) utakaofanyika tarehe 03-06 Februari 2026, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Vyombo vya Habari tarehe 30 Januari 2026, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo amesema kuwa Mkutano huo utatoa fursa kwa washiriki kubadilishana uzoefu, kuimarisha ushirikiano, na kuharakisha matumizi ya zana na teknolojia za kisasa za kilimo kwa ajili ya mageuzi endelevu ya Sekta ya Kilimo nchini na Barani Afrika kwa ujumla.  Mha. Athumani J. Kilundumya, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo naye ameshiriki wakati wa mkutano na waandishi wa habari. 

Washiriki wapatao 1,500 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanatarajiwa kushiriki, wakiwemo Mawaziri wa Kilimo, wadau wa Sekta ya Kilimo, wakulima pamoja na viongozi waandamizi wa Kanda kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).

"Tumetoka mbali sana kwenye kilimo kwa kutumia mikono na jembe la mikono na wananchi wamekuwa wakikosa kulima kwa kiwango kikubwa yaani ‘large scale farming’. Na kushindwa kujingea fursa za kilimo biashara na kilimo chenye tija,” amesema Mhe. Waziri Chongolo. 

Ameongeza kuwa mwelekeo wa Wizara, nchi na ata Dunia kwa ujumla ni msukumo wa kuwa na kilimo cha kinacholimwa kitaalamu na kisasa katika eneo dogo ili kuongeza uzalishaji na kuleta tija.

Aidha, wakati wa mkutano Mheshimiwa Waziri Mkuu Nchemba atazindua awamu ya pili ya Mkakati wa Taifa wa Zana za Kilimo (National Mechanization Strategy Phase Two 2026-2035),ambao utakuwa mwongozo rasmi wa kuongeza tija katika Sekta ya Kilimo kupitia matumizi ya kisasa ya teknolojia.

Waziri Chongolo ametoa hamasa kwa wananchi na wadau wote katika Sekta ya Kilimo kushiriki kikamilifu katika Mkutano huo muhimu kwa maendeleo ya kilimo Barani Afrika.