Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WAZIRI MKUU, MHE. MAJALIWA AZINDUA RIPOTI YA MWAKA YA KILIMO

Imewekwa: 29 Apr, 2025
WAZIRI MKUU, MHE. MAJALIWA AZINDUA RIPOTI YA MWAKA YA KILIMO

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amezindua Ripoti ya mwaka ya Kilimo ya Mwaka (2022-2023, 2023-2024) ikiwa ni ishara ya dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita  chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza na kuimarisha Sekta ya Kilimo nchini.

Uzinduzi huo umefanyika tarehe 27 April 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma wakati akishiriki Kongamano ambalo limejikita katika kujadili Upatikanaji wa Mitaji ya Fedha na Fursa za Maendeleo ya Ushirika kuelekea Uzinduzi wa Benki ya Ushirika Tanzania (COOP Bank Tanzania) tarehe 28 Aprili 2025 itakayozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema “Ripoti inakwenda kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata taarifa sahihi kuhusu hatua iliyofikiwa katika kuendeleza Sekta ya Kilimo na fursa zilizopo katika kuhimiza watu kuingia kwenye kilimo.”

“Ripoti hii haizingatii tuu hali ya uzalishaji wa mazao bali pia inajumuisha maeneo muhimu kama vile lishe, usalama wa chakula, umwagiliaji, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, fursa mbalimbali zinazopatikana, changamoto zilizopo na mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.” ameongeza Waziri Mkuu Majaliwa.

Awali,, akitoa taarifa ya ripoti hiyo, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) ameeleza kuwa ripoti hiyo imelenga kutoa haki kwa Wakulima kujua uwekezaji mkubwa uliofanyika katika Sekta ya Kilimo nchini.

Pia ameeleza kuwa uwepo wa ripoti hiyo kutawawezesha Wakulima na Wanaushirika nchini kushauri na kutoa maoni mbalimbali ili kusaidia kuleta mageuzi makubwa katika Sekta ya Kilimo na itapatikana katika tovuti ya Wizara ya Kilimo.