WAZIRI MKUU NCHEMBA: TANGA HODI, WATENDAJI TATUENI KERO ZA WANANCHI MAENEO YA SEKTA ZENU
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ameanza ziara ya kikazi Mkoani Tanga ambapo ameeleza atatembelea Wilaya zote za Mkoa huo ili kutatua changamoto za wananchi na kuwapatia maendeleo.
Ziara imeanza tarehe 13 Februari 2026 ambapo Waziri Mkuu ameweka jiwe la msingi kwenye Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme cha Msongo wa 132/33 kv Mkata, Handeni mkoani Tanga. Mawaziri alioambatana nao katika ziara ni pamoja na Mhe. Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo; Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Mb), Waziri wa Mifugo na Uvuvi; Mhe. Jumaa Aweso (Mb), Waziri wa Maji; Prof. Riziki Shemdoe (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Lushoto; Mhe Balozi Dk Batilda Burian, Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Viongozi wengine wa Serikali pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo mbalimbali mkoani Tanga.
Mradi huo una gharama za Shilingi Bilioni 44. Aidha, upatikanaji wa umeme jimbo la Handeni kutawezesha wananchi kunufaika na shughuli mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa kiuchumi wakiwemo wakulima. Kadhalika, Kituo hicho kitatoa fursa za ajira 900 na uzalishaji wa zaidi ya tani 200 za madini.
Naye Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) ameongea na kupongeza hatua ya Mkoa wa Tanga katika kuzalisha msimu uliopita zaidi ya tani 1,814,285 za chakula; pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata nyuzi za zao la mkonge mkoani humo. Kuhusu upimaji wa afya ya udongo, ameeleza kuwa tayari vijiji 81 kati ya 91 katika Wilaya la Handeni vimeshapatiwa huduma hiyo ambayo ni bado endelevu katika maeneo mengine nchini.