Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WAZIRI WA KILIMO AHIMIZA KUJENGA MSINGI IMARA WA ZAO LA KOROSHO NCHINI

Imewekwa: 02 May, 2025
WAZIRI WA KILIMO AHIMIZA KUJENGA MSINGI IMARA WA ZAO LA KOROSHO NCHINI

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) ameongoza kikao cha tathmini ya zao la korosho kwa msimu wa mwaka 2024/2025 kilicholenga kujadili mikakati ya kukuza na kuboresha zao hilo muhimu kwa uchumi wa wakulima na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Bashe amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa kila mkulima na msimamizi wa maghala, akieleza kuwa Serikali haitavumilia uzembe wa aina yoyote kwenye mnyororo wa thamani wa zao la korosho.

“Mkulima asiyetazama korosho zake vizuri, asitegemee kula kwa jasho la mwenzake,” amesema kwa msisitizo, huku akiweka wazi kuwa ni lazima kuwe na utaratibu madhubuti wa kutenganisha maghala na kuweka viwango tofauti vya ubora wa korosho zitakazouzwa kwa bei stahiki.

Katika hatua kubwa ya kufufua tasnia ya Korosho, Waziri Bashe ametangaza kuwa Serikali imeanza rasmi kulipa madeni ya nyuma ya wakulima wa korosho yaliyodumu kwa miaka mitatu na huku akieleza Serikali kutarajia kupokea fedha za ushuru wa mauzo ya nje (export levy) na kulipa takribani shilingi bilioni 200. 

Katika kuhakikisha ufanisi zaidi kwenye usimamizi wa mazao, Waziri Bashe ametangaza kuwa Serikali imewaajiri vijana 500 kupitia programu ya vijana na wanawake ya Jenga Kesho iliyo Bora (Build a Better Tomorow - BBT) kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za Sekta ya Kilimo. 

Aidha, Waziri Bashe ameonya vikali kuhusu utoaji wa leseni kwa waendeshaji wa maghala mwaka huu, akisema kuwa Serikali haitatoa leseni kwa mtu yeyote mwenye dosari za kiutendaji au anayekosa uadilifu kwani atakayetaka kuendesha ghala ni lazima aweke pesa taslimu kama dhamana kwa ajili ya kulinda rasilimali za wakulima.

Hatua hizi zinadhihirisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa mkulima anapata haki yake, na tasnia ya korosho inakuwa ya kisasa, yenye tija na inayosimamiwa kwa uadilifu wa hali ya juu.