WIZARA YA KILIMO KWA KUSHIRIKIANA NA UPOV YAENDESHA MKUTANO WA KIMATAIFA WA KUBORESHA KILIMO

Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Hakimiliki za Aina Mpya za Mimea (UPOV) imeendesha mkutano wa kitaalamu wa Kimataifa jijini Arusha tarehe 19 Mei 2025 katika hoteli ya Mt. Meru, ambapo washiriki kutoka Mataifa mbalimbali yapatayo 80 wamehudhuria.
Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Ushirika na Umwagiliaji, Dkt. Stephen Nindi amesema kuwa lengo kuu la mkutano huo ni kuboresha miongozo ya mazao ya kilimo nchini ili kuendana na mahitaji ya sasa na changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta ya kilimo.
Dkt. Nindi amesema kuwa kupitia mkutano huu, wakulima watanufaika kwa kupata mbegu bora zitakazoweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi, hususan katika kipindi cha ukame, pamoja na kukabiliana na magonjwa yanayoharibu mazao.
Aidha, amebainisha kuwa miongozo hiyo ya Kimataifa itatumika zaidi katika mazao mbalimbali ikiwemo miwa, mbegu za mchicha na mazao jamii ya mikunde, kwa lengo la kupata mbegu zenye ubora wa kisasa zitakazotoa mazao mengi kwa muda mfupi.
Vilevile Dkt. Nindi alisisitiza kukamilisha mwongozo wa zao la ngano kutokana na umuhimu wa zao hilo hapa nchini, ambapo takwimu zinabainisha kuwa Tanzania inatumia zaidi ya asilimia 90 ya ngano kutoka nje ya nchi.
Mkutano huu unatarajiwa kuwa chachu ya maboresho katika sekta ya kilimo nchini, hasa katika suala la uzalishaji wa mbegu bora na endelevu kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kutangaza utalii nchini Tanzania.