Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WIZARA YA KILIMO, TOAM WAJADILI MKAKATI WA KILIMO HAI

Imewekwa: 08 May, 2026
WIZARA YA KILIMO, TOAM WAJADILI MKAKATI WA KILIMO HAI

Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Mwamvuli wa Wadau wa Kilimo Hai Tanzania (TOAM) imekutana na Wizara mtambuka kujadili utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kilimo Ikolojia Hai (NEOAS) unaolenga kuendeleza kilimo hicho nchini, tarehe 7 Mei 2026, jijini Dodoma. 

Mwenyekiti wa Bodi ya TOAM na Mshauri wa Rais wa Masuala ya Kilimo na Chakula, Dkt. Mwatima Juma amesema kuwa Kilimo Ikolojia Hai ni suluhisho la uzalishaji wa chakula salama, chenye lishe bora na kinacholinda afya ya udongo pamoja na mazingira. Ameeleza kuwa mfumo huo unasaidia kuongeza rutuba ya udongo, uwezo wa kuhifadhi maji na kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima wadogo.

Aidha, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao, Sehemu ya Uzalishaji wa Mazao na Kuongeza Tija, Bi. Kissa Chawe amesema kuwa mkakati huo unatoa mwongozo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuimarisha masoko ya bidhaa za kilimo hai ndani na nje ya nchi. Aidha, amesema hadi sasa Wizara ya Kilimo imesajili aina 13 za mbegu za asili katika Daftari la Mbegu la Taifa ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono maendeleo ya Kilimo Ikolojia Hai nchini.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TOAM, Bw. Bakari Mongo amesema ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau utaimarisha mazingira ya biashara na kuongeza mafanikio kwa wakulima wa kilimo hai. Naye Meneja Utendaji wa TOAM, Bi. Sandra Haule amesema utekelezaji wa mkakati huo umeongeza ushiriki wa wakulima, taasisi za utafiti, mashirika ya kiraia na sekta binafsi katika kuendeleza Kilimo Ikolojia Hai nchini.

Washiriki wa kikao hicho wamekubaliana kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha Mkakati wa Taifa wa Kilimo Ikolojia Hai unatekelezwa kwa mafanikio kwa manufaa ya wakulima, mazingira, afya ya wananchi na uchumi wa Taifa.