Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WIZARA YA KILIMO YAPOKEA UJUMBE KUTOKA POLAND KUJADILI USHIRIKIANO WA KILIMO

Imewekwa: 08 Feb, 2026
WIZARA YA KILIMO YAPOKEA UJUMBE KUTOKA POLAND KUJADILI USHIRIKIANO WA KILIMO

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb), amepokea ujumbe kutoka mashirika ya KUKE na FASPOL ya nchini Poland, ulioongozwa na Bw. Janusz Wladyczak, Rais wa Bodi ya Shirika la Bima ya Mikopo ya Usafirishaji (KUKE), akiambatana na Bw. Marcin Kaleta, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya FASPOL, tarehe 4 Februari 2026, jijini Dodoma.

Mazungumzo hayo yalilenga zaidi kuimarisha usalama wa chakula, hususan katika ujenzi wa vihenge vya kisasa vya kuhifadhia mazao ya chakula, hatua itakayosaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhe. Silinde alibainisha maeneo kadhaa ya ushirikiano ikiwemo kuanzishwa kwa vituo binafsi vya kukodisha zana na mashine za kilimo ili kuongeza tija kwa wakulima, kuimarisha na kupanua miundombinu ya umwagiliaji, pamoja na uwekezaji katika uzalishaji wa mbolea kwa lengo la kuongeza matumizi ya mbolea kwa wakulima nchini.

Aidha, Mhe. Silinde alieleza kuwa zipo fursa nyingine muhimu za ushirikiano katika uwekezaji wa viwanda vya uchakataji wa mazao ya kilimo, ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao kwa mfumo wa baridi, pamoja na uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa zao la ngano, ikiwemo uzalishaji wa mbegu bora kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa ndani.

Tanzania na Poland zina ushirikiano wa kihistoria tangu mwaka 1962 katika nyanja mbalimbali huku ushirikiano wake katika Sekta ya Kilimo ulianza mwaka 2015.  Tangu ushirikiano huo kuanza, Poland imekuwa ikiagiza kutoka Tanzania bidhaa za mazao mbalimbali yakiwemo kahawa, chai, kakao, korosho, tumbaku, pamba pamoja na mbegu za mafuta.