Skip to main content
Machapisho
Miongozo
Progamu
Swahili
ASDP II

Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II)

Sekta ya kilimo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Asilimia 90 ya ardhi ya Tanzania hulimwa na wakulima wadogo. Sekta inatoa ajira kwa asilimia 65.5 na huchangia asilimia 29.1 ya pato la Taifa, asilimia 30 ya soko la nje na asilimia 65 ya malighafi za viwanda. Ili kuendeleza sekta ya Kilimo, Serikali kupitia Wizara za Sekta ya Kilimo (ASLMs)1 na kwa kushirikiana wa wadau wa sekta imeandaa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya pili (ASDP II). ASDP II ni muendelezo wa awamu ya kwanza ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP I) iliyotekelezwa kuanzia 2006/2007 hadi 2013/2014. 

ASDP II ni mpango wa miaka kumi utakaotekelezwa kuanzia 2017/2018 hadi 2017/2028 kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano. Utekelezaji wa awamu ya kwanza utaanza 2017/2018 hadi 2022/2023. ASDP II inalenga katika kuleta mageuzi ya Sekta ya kilimo (kilimo, mifugo na uvuvi) ili kuongeza uzalishaji na tija, kufanya kilimo kiwe cha kibiashara zaidi na kuongeza pato la wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha yao, uhakika wa usalama wa chakula na lishe, na kuchangia katika pato la Taifa.

ASDP II imeandaliwa kwa kuzingatia mikakati yote ya Taifa: Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025; Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu (2012-2021); Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016-2021); Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo (2015) na Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo (Tanzania Agriculture and Food Security Investment Plan – TAFSIP 2011). 

Pia programu hii imezingatia mambo makuu tuliyojifunza katika utekelezaji wa ASDP I ili kukabiliana na mapungufu na changamoto za sekta ya kilimo na kuongeza kasi ya ukuaji wa pato la Taifa, kuboresha ukuaji wa pato la wakulima wadogo na kuwa na uhakika wa usalama wa chakula ifikapo 2025.

Pakua Faili: