Skip to main content
Habari na Matukio

WAZIRI BASHE ASHIRIKI KUKABIDHI MRADI WA LUICHE

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) ameshiriki katika kukabidhi mradi wa umwagiliaji wa Bonde la  Luiche, mkoani Kigoma lenye ukubwa wa hekta 3000 kwa mkandarasi M/S CRJE (East Africa) LIMITED ya Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa bwawa na skimu ya umwagiliaji leo tarehe 21 Julai 2024.

Akitoa salamu za Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Mkurugenzi Mkuu Bw. Raymond Mndolwa ameeleza kuwa mradi una gharama za Shilingi Bilioni 65.16 ambapo utahusisha ujenzi wa bwawa, mfereji mkuu wa kuingiza  maji, uchimbaji wa mitaro ya kutoa maji katika mashamba, ujenzi wa barabara za mashambani, nyumba za watumishi, ofisi za wahandishi pamoja na ujenzi wa ghala na kusimika mashine ya kukoboa mpunga. 

“Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imejipanga na tuko tayari kuhakikisha wananchi wa Bonde la Luiche wananufaika na mradi huu.  Tunampongeza sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kukuza kilimo cha umwagiliaji,” amesema Bw. Mndolwa. 

“Mradi huu utakapokamilika utanufaisha wakulima zaidi ya tisa kwa kumwagilia eneo lenye ukubwa wa hekta 3000 kwa skimu ya Bonde la Luiche,” amesema Waziri Bashe.  Pia ameongeza kuwa mradi huu ni muhimu ambao utanufaisha wananchi wa kata za Kagera, Simba na Mungonya katika Mkoa wa Kigoma.  

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. CGF (mstaafu) Thobius E. M. Andengenye amesema zaidi ya Shilingi Bilioni 60 zilizotengwa kwa ajili ya mradi huu ni hatua muhimu ya kuwajali wananchi wa Luiche na Kigoma kwa ujumla.  “Nikupongeze Mhe. Waziri Bashe kwa kutafsiri maoni ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha ndoto ya mradi huu inaanza kutekelezwa,” amesema Mhe. CGF Andengenye. 

 

Kwa upande mwingine, Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Ng’enda Kirumbe ametoa shukran kwa Wizara ya Kilimo kwa kuleta mradi huu ambao umekuwa unazungumziwa tangu Uhuru.  “Mradi huu unakuja kututhibitishia sisi na vizazi vyetu mkono kwenda kinywani na kuongeza mzunguko wa fedha kupitia miradi wa kilimo cha umwagiliaji,” amesema Mhe. Kirumbe.

 

Mkoa wa Kigoma una zaidi ya hekta 120,000 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, ambapo eneo linalomwagiliwa ni hekta 9,070 huku kuna mabonde na skimu jumla 59.