Skip to main content
Habari na Matukio

KUSAYA AWATAKA WAKANDARASI WA UJENZI WA MAGHALA KUMALIZA KWA WAKATI

 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ametembelea miradi  11 iliyopo chini ya  Mradi wa Kuendeleza zao la mpunga  ( ERPP ) mkoani Morogoro ikiwa ni ziara yake ya kikazi. Miradi hiyo ni pamoja na maghala yaliyopo Mbogo Komtonga , Kigugu, Msolwa Ujamaaa ,Njage  na skimu ya umwagiliaji ya Kigugu,  Mvumi, Kilangali na  skimu ya Msolwa ujamaa.

Katika ziara hiyo Bw.Kusaya amewasisitiza wakandarasi kumaliza kazi mapema kwani wananchi wanahitaji kutumia miradi hiyo ikiwa ni zawadi kutoka kwa Mhe. Rais John Magufuli na pia amewataka wananchi kuitunza miradi hiyo ikiwa ni pamoja na kupanga namna ya kuitunza miradi hiyo kwa kuchangia 5% kwa kila mmoja.

“Nia yetu ni kulitumia mwezi ujao wa saba mwanzoni,ikifika tarehe 30/06/2020 unikabidhi ghala na uondoke ili hili ghala liwe mikononi mwenu wananchi “ alisema Kusaya

Aidha, Kusaya amesema ujenzi huu wa maghala utasaidia  kuhifadhi mazao kwa njia sahihi kwani kumekuwa na njia mbaya za kuhifadhi mazao na kupelekea kuwepo kwa madhara ya Sumukuvu. Naye mkandarasi wa ghala la Komtonga Bw.Fikiri Andrew amesema kwa upande wake amefikia 98% ili akamilishe mradi huo na atakabidhi kazi tarehe 1/7/2020.

Katika miradi hiyo fedha zitakazobaki zitatumika katika kutengeneza barabara,kuweka chaga, chanja kwa ajili ya kuanikia mazao na kujenga uzio.