Skip to main content
Habari na Matukio

MHANDISI MTIGUMWE AITAKA BODI YA KAHAWA KUONGEZA UZALISHAJI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe ameitaka Bodi ya Kahawa ambayo ni Taasisi ya Serikali iliyopewa jukumu la kusimamia sekta ya Kahawa nchini kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa Kahawa nchini kwani  Kahawa ni miongoni mwa mazao ya kipaumbele.

Mhandisi Mtigumwe ametoa rai hiyo wakati akizungumza na Wafanyakazi wa Bodi ya Kahawa Mara baada ya kutembelea Ofisi za Bodi hiyo zilizopo Mtaa wa Railway, Kata ya Mawenzi Katika Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro.

Alisema kuwa Mwaka 2011 wadau waliandaa na kupitisha mkakati wa miaka 10 wa maendeleo ya Kahawa ambayo lengo kuu ilikuwa ni kuongeza uzalishaji hadi kufikia Tani 80,000 Mwaka 2017 na Tani 100,000 Mwaka 2021 lengo ambalo halijafikia na bado uzalishaji ni mdogo hivyo kuongeza uzalishaji linapaswa kuwa jambo la haraka iwezekanavyo.

Katibu Mkuu alimuelekeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu/Mkurugenzi wa Ubora wa Kahawa na Uhamasishaji Masoko Kufanya Utafiti ili kubaini nini chanzo cha uzalishaji mdogo wa kahawa iwapo Wananchi kutotunza vizuri kahawa yao, hali ya hewa na udongo au mbegu sio nzuri zinazotumika.

Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali inajipanga kwa kampeni kubwa kutoa elimu kwa Wananchi juu ya kufahamu umuhimu wa kulima kwa wingi mazao ya chakula na biashara ikiwemo zao la kahawa.

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema miongoni mwa sababu ambazo huchangia uzalishaji mdogo katika mazao mbalimbali nchini huwa ni pamoja na wananchi kuchanganya mazao wakati wa kupanda jambo ambalo sio rafiki sana katika Kilimo, sambamba na kutoacha nafasi kati ya mche na mche.

Mhandisi Mtigumwe aliitaka Bodi ya Kahawa kufanya utafiti wa maeneo ambayo kahawa inastawi kwa wingi ili kuongeza sehemu za kuzalisha zao hilo ili kufikia uzalishaji wa kiwango kikubwa tofauti na ilivyo hivi sasa.

Hata hivyo amesema kuwa atazishughulikia haraka iwezekanavyo changamoto za uzalishaji, changamoto za ubora, masoko sambamba na changamoto nyengine.

Majukumu ya Bodi ya Kahawa ni pamoja na usimamizi wa sheria namba 23 ya marekebisho yake ya Mwaka 2009 na kanuni za Kahawa 2013 sambamba na kuratibu Majukumu Shirikishi (Shared Functions) baina ya Serikali na Wadau.