Skip to main content
Habari na Matukio

NFRA YATANGAZA UNUNUZI NA UHIFADHI WA MAZAO KIDIGITALI

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imesema itafanya manunuzi ya mazao kutoka kwa wakulima na kuyahifadhi kwa kutumia pia mfumo wa kidigitali.

Hayo yamesemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Dkt. Andrew Komba baada ya hafla fupi ya kusaini Randama ya Mashirikiano kati ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB ) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) iliyofanyika tarehe 5 Juni 2024, jijini Dodoma.  Hafla hiyo imeshuhudiwa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb).

Aidha, Dkt. Komba amesema sehemu ya makubaliano ya randama hiyo ni ununuzi wa mahindi kutoka NFRA na CPB  utakaoanza  kati ya tarehe 15 hadi 20 Julai 2024.

Amesema mkataba huo una thamani ya  Dola za Marekani milioni 22 ambao utahusisha  ununuzi wa tani 60,000 za mahindi kutoka kwa wakulima. Hatua hiyo itatatua changamoto ya soko na bei kwa wakulima kwani Serikali itatangaza bei elekezi ya ununuzi wa mazao hayo.

Pia, Dkt Komba amesema kwa mwaka 2024 kupitia NFRA kwa kushirikiana na WFP  itaongeza vituo vya ununuzi ili kuweza kuwafikia wakulima wengi kwa wakati na  umbali mfupi katika zoezi la ununuzi.

Kwa upande wake Mwakilishi wa WFP, Bi. Sarah Gordon-Gibson ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na WFP katika kuendeleza sekta ya kilimo.

Bi. Gordon-Gibson amesema kati ya Mwaka  2011 hadi 2023, WFP imenunua  zaidi ya tani 223,000 za mahindi meupe na tani 4,000 za mtama kwa thamani ya jumla ya zaidi Dola za Marekani milioni 60 kutoka NFRA.

Viongozi wengine waliohudhuria ni Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo Bw. Obadia Nyagiro, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. Mariam Ditopile Mzuzuri (Mb), Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge pamoja na  Mkurugenzi Mkuu wa CPB, Bw. Patrick Mongella.