Skip to main content
Habari na Matukio

Rais Samia alivyokinadi kilimo Jukwaa la Uchumi Duniani

Na Evance Ng’ingo

RAIS Samia amewahakikishia wadau wa maendeleo duniani kuwa Tanzania
itafanikisha ukuaji wa sekta ya kilimo kwa asilima 10 ifikapo mwaka
2030 ikilinganishwa na ukuaji wa sasa wa asilimia 3.6.

Rais Samia amebainisha hayo kwenye Mkutano wa Jukwaa la Uchumi la
Dunia (WEF) jijini Davos nchini Uswisi ambapo amegusia namna ambavyo
sekta ya kilimo inavyotarajia kukua huku akibainisha mikakati
inavyoendelea kutekelezwa na serikali kupitia wizara ya kilimo.

Baadhi ya mambo ambayo Rais Samia ameyaahinisha  ambayo yanayotazamwa
kama nguzo katika kuchochea ukuaji huo ni pamoja na  mageuzi
yanayoendelea kwenye sekta ya kilimo kama vile uanzishwaji mpango wa
vijana kujikita kwenye kilimo na ongezeko la kiwango cha bajeti katika
sekta hiyo.

Pia amegusia kuongezwa kwa bajeti ya kilimo kwa mwaka wa fedha 2022-
2023 kuwa imeongezeka mara nne ikilinganishwa na iliyopita.

Ongezeko hilo limeifanya serikali kuwa na uwanja wa kuanza kutoa
ruzuku ya mbolea kwa wakulima, ruzuku ambayo itamwezesha mkulima
kupata mbolea kwa bei nafuu hasa wakati huu ambako bei yake iko juu
kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo vita vya Urusi na Ukraine.