Skip to main content
Habari na Matukio

RAIS SAMIA AZIDI KUINADI TANZANIA KIUCHUMI

Na Tagie Daisy M.

Wizara ya Kilimo, Lindi.

Ziara ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mikoa ya Mtwara na Lindi imezidi kuipaisha Tanzania kiuchumi kutokana na shughuli za Kilimo, Uvuvi na Mifugo wanazozifanya wananchi. 

Ziara hizo zilianza tarehe 15 Septemba 2023 na kuhusisha upande wa Mtwara uzinduzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bandari ya Mtwara, Uwanja wa Ndege, Ghala la Chakula na Chujio la Maji Mangamba.   Mkoa wa Lindi, kumefanyika uwekaji wa jiwe la msingi kwenye bandari ya kisasa Kilwa, uwekaji jiwe la msingi kwenye shule ya sekondari ya wasichana, uwekaji wa jiwe la msingi barabara ya Ruangwa Nanganga yenye kilomenta 53.2 na jiwe la msingi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi. 

Aidha, ziara hizo pia zimehusisha taarifa ya minara 54 ya mawasiliano itakayojengwa katika Mkoa wa Lindi ambapo kumekuwa na changamoto ya mawasiliano.  Taarifa hiyo ilitolewa na Mhe. Nape Nnauye (Mb), Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia Habari. 

Kwenye Kilimo, Mhe. Rais Samia amehamasisha wakulima wa Mikoa ya Kusini kuzalisha chakula kwa wingi na mazao mengine kuanza kuyalima kwa matumizi ya biashara kama mbaazi na Ufuta.  Sambamba na hilo, Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo naye alitoa hamasa kwa Wakulima na kuwaeleza jitihada za Serikali za kujenga Kongani ya Viwanda vya kubangua korosho kwa dhamira ya kuongeza thamani ya zao hilo kibiashara kwa wakulima. 

Ziara ya Mhe. Rais Samia imeshirikisha Mawaziri wa Kisekta, Viongozi mbalimbali kutoka Taasisi za umma na Binafsi, viongozi kutoka Mikoa, Wilaya na Halmashauri. 

Katika nafasi nyingine, Mhe. Waziri Bashe aliwaeleza wananchi wa Lindi kuwa Serikali imepanga kuchimba mabwawa 7 makubwa ili kuwezesha kilimo cha umwagiliaji.  Kuhusu zao la korosho, Mhe. Waziri Bashe alieleza kuwa Wizara ya Kilimo imepokea maelekezo ya Mhe. Rais Samia ambapo nao Mkoa wa Lindi utajengewa kiwanda cha kubangua korosho kama Mkoa wa Mtwara. 

Kuhusu Mazao yanayolimwa kwenye Mkoa wa Lindi, Mhe. Waziri Bashe alieleza kuwa Mkoa wa Lindi utapatiwa miche laki 5 bure ya minazi ili Wakulima waweze kupanda na kuanza kuvuna baada ya miaka minne.  Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia Wakulima kukidhi mahitaji ya nazi nchini. 

“Wizara ya Kilimo pia itatoa tani 30 za mbegu za ufuta kwa Wakulima wa Lindi na tayari nimeshatoa maelekezo kwenye Bodi ya Korosho na Vyama vya Ushirika ili zoezi hilo lianze,” aliongeza Mhe. Waziri Bashe. 

Mhe. Rais Samia anatarajiwa kuhitimisha ziara yake Mkoa wa Lindi tarehe 20 Septemba 2023 ambapo atatembelea Mradi wa Maji uliopo Mchinga, Lindi na kuelekea kijiji cha Somanga ambapo ataongea na wananchi mkoani humo Lindi.