Skip to main content
Habari na Matukio

RAIS SAMIA AZINDUA NA KUGAWA VITENDEA KAZI KWA MAAFISA UGANI KILIMO 7,000 KOTE NCHINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni aligawa vitendea kazi kwa Maafisa Ugani Kilimo zaidi ya 7,000 katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma na kuhudhuliwa na Viongozi wa kitaifa, kimataifa na Wageni wengine zaidi ya 3,000.

Akizungumza katika uzinduzi huo Rais Samia amesema ni muhimu kila Afisa Ugani akafanye kazi kwa bidii na kutumia vifaa walivyopatiwa kwa malengo mahususi.

Vitendea kazi walivyopewa Maafisa Ugani hao ni pamoja na pikipiki moja, kifaa maalum cha kupimia afya ya udongo (Soil Scanner), koti maalum la kujikinga na mvua, kifaa cha kupuliza dawa ya kuua wadudu waharibifu mashambani (Boom sprayer pump 20 lts), viatu maalum vya shambani (Gun booties).

"Ombi la Waziri kuwaachia pikipiki baada ya miaka miwili sio mbaya ila tutakwenda kuwapima kwa utendaji kazi wenu kwanza, mkifanyakazi kwa bidii na kuzitunza pikipiki hizo hatuna budi kuwaachia kama alivyoomba Waziri wa Kilimo,"amesema Rais Samia.

Aidha Rais Samia amewataka Vijana wa Tanzania kuingia katika Sekta ya Kilimo kwani hawatajuta na badala yake watatengeneza fedha nyingi na za halali.

"Sekta ya Kilimo imeendelea kuwa muhimu na kuleta maendeleo ndani ya Nchi yetu hivyo nikuchuke muda huu kuwataka vijana wetu kuhakikisha wanawekeza kupitia Kilimo kwani ni biashara ambayo inamatunda mazuri,"amesisitiza.

Pia amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wakutosha ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira wezeshi kwa Wizara ya Kilimo na Mashirika Binafsi, kuiendeleza Sekta ya Kilimo.

Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza Wizara ya Kilimo na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora kupitia upya na kuufanyia mabadiliko muundo wa Tume ya Umwagiliaji ili kuhakikisha Tume inakuwa na ofisi katika kila wilaya hapa nchini.

Aidha, Rais Samia pia ameiagiza Wizara Kilimo ili ishirikiane na Wizara ya Fedha na Mipango, kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo ambao utachangiwa na tozo maalum kwenye mazao ya kilimo, Mfuko Mkuu wa Serikali na Wadau wa Maendeleo kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji kwenye Sekta hiyo iliyoajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wote. 

Rais Samia amesema Mfuko huo utakuwa na majukumu ya kugharamia pembejeo za kilimo kama ilivyofanyika kwenye korosho, pamba na tumbaku ili mfuko huo utumike kupunguza utegemezi kwenye ruzuku pindi pembejeo zinapopanda bei. 

Kwa upande mwingine, Rais Samia ameagiza mashamba yote ambayo yapo chini ya ofisi ya Msajili wa Hazina kufufuliwa na kuanza kutumika kwa kushirikiana na Sekta Binafsi kwa mfumo wa kukodisha ardhi kwa muda mrefu.

Hali kadhalika, Rais Samia ameitaka Wizara ya Kilimo kuweka msukumo kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula na kuwa ya kibiashara, ikiwemo mazao ya mboga, matunda na viungo pamoja na mazao ya kimkakati ili kukidhi mahitaji ya ndani na kuuza ziada nje ya nchi.

Rais Samia amesema Sekta ya kilimo nchini imeendelea kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa taifa ambapo kwa mwaka 2020 Sekta ya Kilimo ilikua kwa asilimia 4.9, na kuchangia kwa asilimia 26.9 katika pato la taifa, kuchangia kwa asilimia 61.1 katika kutoa ajira kwa Watanzania na kuchangia kwa asilimia 65 ya malighafi za viwandani.