Skip to main content
Habari na Matukio

SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA MIFUMO YA UUZAJI WA MAZAO NCHINI

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imesema inaendelea kuimarisha mifumo ya uuzaji wa mazao nchini ili kuongeza ushindani na kumunufaisha mkulima.

Hayo yamesemwa leo Novemba 7, 2023 na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) wakati akijibu swali la Mbunge wa Kyela, Mhe. Ally Jumbe Mlaghila kuhusu mfumo wa uuzaji wa zao la Kakao ili kumnufaisha mkulima baadala ya Wafanyabiashara wachache.

Mhe. Silinde ameeleza kuwa zao la Kakao huuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani chini ya utaratibu wa minada ambao huratibiwa na Vyama vya Ushirika. Mfumo huo ulianza kutumika mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo bei ya Kakao imeendelea kuimarika kulingana na hitaji la soko.

“Wastani wa bei ya Kakao kwa kilo kuanzia msimu wa 2018/2019 ilikuwa shilingi 4,611 na mwaka wa fedha 2019/2020 ilikuwa shilingi 5,034 na mwaka wa fedha 2020/2021 ilikuwa shilingi 4,818 na mwaka wa fedha 2021/2022 ilikuwa 4,711.  Hadi kufikia tarehe 23, Oktoba msimu wa mwaka wa fedha 2023/2024 wastani wa bei ya Kakao kwa kilo imefikia shilingi 8,079,” ameeleza Mhe. David Silinde.

Aidha, Mhe. Silinde amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati ya uwekezaji katika zao la kahawa nchini na itaendelea kuwasaidia wakulima katika maeneo yote nchini yanayolima zao hilo.