Skip to main content
Habari na Matukio

SERIKALI YAOKOA TANI 556.5 YA MBEGU ZA NAFAKA KWA KUDHIBITI KWELEA KWELEA – BASHE.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe amepokea ndege ya kunyunyizia  dawa aina ya beaver 5Y DLD kwaajili ya kudhibiti visumbufu vya mimea aina ya kweleakwelea ambao wana uwezo wa kuharibu gramu 10 za nafaka kwa ndege mmoja kila siku.

“Kwa kawaida mikoa 12 ya Tanzania bara hupatwa na milipuko ya kwelea kwelea kila mwaka kutokana na tabia ya kwelea kwelea kuwa na uwezo wa kuharibu gramu 10 za nafaka kwa ndege mmoja kila siku.,kundi dogo lenye idadi ya wastani wa ndege milioni moja lina uwezo wa kuharibu tani 10 kwa siku.” Alisema Bashe

Mhe.Bashe ameendelea kusema kwamba uvamizi wa kwelea kwelea katika mashamba husababisha wastani wa uharibifu wa asilimia 30 kwa mazao yetu kila mwaka, na pia visumbufu vya mimea hususan vya milipuko ni tishio kubwa la usalama wa chakula hapa nchini.

Hata hivyo Tanzania husumbuliwa kila mwaka na aina nne ya visumbufu , ambavyo ni ndege aina ya kwelea kwelea, Viwavijeshi,Nzige na Panya. Visumbufu hivi vina tabia ya kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine vikifuata chakula.Ili kuweza kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na kudhibiti visumbufu hivyo  Mhe. Bashe amesema Wizara inatarajia kuanzisha Kitengo cha Kilimo anga ambacho kitafanya kazi hii.

Aidha, katika msimu 2019/2020  jumla ya ndege milioni 55.65 wameuwawa na kuweza kuokoa tani   556.5 za mbegu za nafaka kwa siku. Pia kwa ajili ya udhibiti wizara imetumia jumla ya lita 1,905 za kiuatilifu (FenthionULV 60%) na lita 5,716 za mafuta JET A-1.

 Kwa musimu wa 2019/2020 ndege hawa wamedhibitiwa katika Mikoa ya Mwanza; (wilaya ya Sengerema), Mkoa wa Shinyanga; (wilaya ya Kishapu na Shinyanga DC), Tabora; (wilaya ya Igunga, Uyui na Nzega), Mkoa wa Geita;  (wilaya ya Geita DC na Chato).

Mkoa wa Dodoma; (wilaya ya Dodoma jiji,  Bahi na Kondoa), Mkoa wa Singida; (wilaya ya Singida DC, Manyoni na Ikungi).

 Mkoa wa Iringa; (wilaya ya Iringa DC) na Mkoa wa Mbeya (wilaya ya Mbarali) na   Mkoa wa Manyara (wilaya ya Hanang).

 Bashe amemalizia kwa kusema kwamba Udhibiti umefanywa na Wizara Kilimo kwa kushirikiana na shirika la Kimataifa la Kudhibiti Nzige wa Jangwani (Desert Locust Control Organization for East Africa) kutoka Nairobi Kenya kwa kutumia ndege ya kunyunyizia aina ya beaver 5Y DLD ambapo ilianza kufanya kazi Dodoma na inaelekea Mvomero Morogoro kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.