SILINDE AMPONGEZA RAIS SAMIA KWA UTEKELEZAJI WA VITENDO MRADI WA BBT
Naibu waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) amempongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utekelezaji wa vitendo wa miradi ya Jenga Tanzania iliyo Bora (Build a Better Tomorrow - BBT) nchini.
Amesema miradi hiyo itasukuma malengo ya Serikali katika kuhakikisha usalama wa chakula nchini, ajira kwa vijana pamoja na kuhakikisha ukuaji wa kipato kwa Watanzania.
Mhe. Silinde amesema hayo tarehe 3 Oktoba 2023 katika ziara ya kikazi alipotembelea moja kati ya mradi wa BBT uliopo Chinangali, mkoani Dodoma.
"Mnapoona mpaka hatua hii tuliyofikia ya mradi huu, hii inaonesha msukumo na maono ya Mhe. Rais katika utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, kwa hiyo tupo hapa kujionea matunda ya utekelezaji wake unaoendelea,” amesema Mhe. Silinde.
"Tunataka Tanzania tuwe wazalishaji wakubwa ikiwezekana Afrika na Dunia kwa ujumla, ndiyo maana tumekuja na miradi ambayo mwananchi wa kawaida, ukiacha vijana wa BBT, awe na uwezo wa kulima kwa misimu miwili mpaka mitatu ndani ya mwaka mmoja", ameongeza Mhe. Silinde wakati wa ziara ya ukaguzi wa eneo la mradi wa BBT uliopo Chinangali.
Ameeleza kuwa kupitia mabadiliko makubwa ya Kilimo yanayokwenda kufanyika, ongezeko la ajira nchini linakusudiwa kufikia ajira million 8, sehemu kubwa ya ajira hiyo ni kupitia kilimo cha kisasa.
Ziara hiyo ni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo ambapo Waheshimiwa Wabunge wameweza kuona utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Wizara na Sekta ya Kilimo kwa ujumla. Ziara hiyo inaendelea pia katika Mikoa ya Tabora, Arusha, Iringa na Mbeya