SUA vinara kwa wabobezi wa Kilimo hai na Kilimo ikolojia Tanzania
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimeendelea kuwa kinara katika kufanya tafiti na kuzalisha wataalamu wa masuala ya Kilimo Hai hata kabla ya kuazishwa kwa taasisi na mashirika mbalimbali ambayo yanahamasisha na kusisitiza matumizi na faida za kilimo hai nchini Tanzania.
Hayo yamesemwa na Mtafiti Mbobezi kwenye tafiti za Kilimo Hai kutoka SUA Prof. Kalunde Sibuga wakati akiwasilisha maelezo yake kuhusu mchango wa SUA katika kutekeleza maazimio ya Mkutano wa kwanza wa kitaifa wa Kilimo hai wa mwaka 2019 kwenye mkutano wa pili unaoendelea Jijini Dodoma.
“Katika shahada ya kwanza tumekuwa na mtaala wa Kilimo Hai Hata kabla ya Mkutano wa mwaka 2019 na mtaala ulilenga wanafunzi wanaochukua shahada ya Kilimo pamoja na ile ya Bustani na Mbongamboga, na huu mtaala bado upo kwahiyo tulianza zamani” Alifafanua Prof. Sibuga.
Amesema kila mwaka nchini Uganda kumekuwa kukiendshwa mafunzo ya muda mfupi ya Kilimo Hai na Chuo kwa kutambua umuhimu wake kimekuwa kikiwapatia wanafunzi wake ruhusa ya kwenda kuhudhuria na kuonea ujuzi na kisha kurejea kuendelea na masomo na mitihani yao.
Prof. Sibuga amesema kuwa kupitia pia Mradi wa kujenga vyuo imara (Building Stronger Universities) wamefanikiwa kuwezesha kupatikana kwa mtaala kwa Wanafunzi wa Shahada ya Uzamivu mtaala ambao wadau mbalimbali walishirikishwa katika kuuboresha na kuwezesha kuwapa nafasi ya kusoma darasani lakini pia kuwepo kwa sehemu ya utafiti .
Sambamba na hilo pia tayari wanao mtaala mwingine wa Shahada ya Uzamili ambao umeshatengenezwa na sasa upo kwenye hatua mbalimbali za kuboreshwa na wadau ili uweze pia kupitishwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kabla ya kuanza kutumika.
Pia Mtafiti huyo amesema pamoja na mambo hayo lakini SUA na watafiti wake wamekuwa na miradi kadhaa ya kilimo hai na kilimo ikolojia kama mradi wa uzalishaji na ukuaji wa mnyororo wa thamani za mazao ya kilimo Hai ambao walikuwa wanashirikiana na watafiti wengine wa afrika mashariki ambapo vijana wawili walipata shahada za Uzamili na wengine wawili walipata shahada zao za uzamivu.
Prof. Sibuga amesema kutokana na umuhimu huo hivi sasa SUA ina takribani miradi minne ya kilimo Hai ambayo inatekelezwa kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi Kitovu cha Kilimo Ikolojia Tanzania Prof. Dismas Mwaseba kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo SUA akitoa mrejesho wa mjadala wa mifumo wa chakula amesema kuwa walifanikiwa kufanya mkutano ambao wadau mbalimbali walishiriki katika kuongeza mapokeo ya kilimo Ikolojia na kilimo Hai nchini.
Prof.Mwaseba amesema mambo mbalimbali yalijadiliwa lakini hasa ni katika Utafiti,Sera, Uenezwaji wa matokeo na ushawishi ambapo amesema katika sera yalijadiliwa mambo mengi lakini ilibainika kuwa Sera za kilimo nchini hazijazungumzia maswala ya Kilimo Ikolojia na Kilimo Hai.
“Wadau wamependekeza kwenye mkutano huo kuwa kwenye swala la utafiti na mafunzo iwepo mitaala kwenye taasisi za elimu hasa vyuo vya Kilimo ambayo itafundisha maswala ya Kilimo Ikolojia na Kilimo Hai kwa mapana yake na kuwa kuna haja ya kufanya utafiti kubainisha mahitaji ya wadau mbalimbali kwakuwa sasa tafiti zilizopo zimegusa wadau maalumu tu hasa wa Kilimo cha mboga” Alieleza Prof. Mwaseba.
Mratibu huyo wa Mradi wa Kitovu cha Kilimo Ikolojia amesema pia kuwa wadau wanapendekeza kuwepo na ushawishi ambao utatokana na Ushahidi wa Kiutafiti na hasa zile teknolojia mbazo zimethibitika kwa ubora wake na utangazaji wa bidhaa za Kilimo ikolojia uzingatie mahitaji ya soko.
Prof. Mwaseba alibainisha kuwa Wadau wa mkutano huo walisema Kitovu cha Kilimo Ikolojia kinaweza kufanikisha maswala mbalimbali ya sera,uwezeshaji pamoja na utafiti ambapo katika kikao hicho wadau walipendekeza sasa kwakuwa mradi unaisha basi kianzishwe kitovu cha Kilimo Ikolojia na wadau wote waweze kujiunga na kuchangia katika kushughukikia maswala mbalimbali ambayo yanakigusa Kilimo hicho nchini.
Katika Kongamano hilo la pili la kitaifa la kilimo Hai nchini, Wanafunzi mbalimbali wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wanaofanya Tafiti zao katika maswala ya Kilimo Ikolojia na Kilimo Hai wamepata nafasi ya kuwasilisha matokeo ya Tafiti zao na kujadiliwa na wadau hao lakini pia watafiti wa SUA nao wamewasilisha na kushiriki kwenye mijadala mbalimbali kuonesha ushiriki wao katika kuchangia ukuaji wa kilimo Hai Nchini.
Na. Calvin Gwabara - Dodoma