Skip to main content
Taarifa kwa Vyombo vya Habari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU TISHIO LA KUVAMIWA NA NZIGE WA JANGWANI MSIMU WA 2019/2020

Dodoma, 29 Januari, 2020

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb) anautaarifu umma na wananchi kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kufuatiliaji viashiria vya uwepo wa Nzige wa Jangwani (Locust Desert) na udhibiti wake kutoharibu mazao ya wakulima nchini.

Katika taarifa yake Mhe. Hasunga amesema “hadi sasa hakuna uthibitisho wa kitaalam kuhusu uwepo wa Nzige wa Jangwani nchini Tanzania” na kuongeza kuwa Serikali imejipanga kuwadhibiti nzige hao endapo wataingia nchini. Hadi sasa Serikali ina lita 7,000 za viuatilifu kwa ajili ya tahadhari ya kukabiliana na tishio hilo na ununuzi wa viuatilifu vingine zaidi unaendelea kufanyika.

Wizara ya Kilimo inaendelea kuchukua tahadhali kuhakikisha visumbufu vya mazao ya kilimo kama Nzige Wekundu, Ndege waharibifu wa nafaka aina ya Kwelea kwelea, panya na Kiwavijeshi Vamizi zinaripotiwa na kudhibitiwa kwa haraka.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo tishio la Nzige wa Jangwani limeripotiwa katika nchi za Eritrea, Ethiopia, Somalia, Sudan na Kenya hivyo kuwepo uwezakano wa Tanzania kuvamiwa na Nzige hao.

Serikali inatoa wito kwa wataalam wa kilimo na Maafisa Ugani nchini kutoa taarifa za viashiria au uwepo wa Nzige wa Jangwani kwenye maeneo ya kilimo, malisho na uoto wa asili ili hatua za haraka za kuwadhibiti zichukuliwe na kuwezesha wakulima kuvuna mazao yao kwa wingi na nchi yetu kuendelea kuwa na uhakika wa chakula.

Imetolewa na;

Katibu Mkuu,

Wizara ya Kilimo,

DODOMA