Skip to main content
Habari na Matukio

“Tafiti za kilimo zilete mageuzi ya biashara kwenye kilimo”- Katibu Mkuu Mweli

Watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) wametakiwa kuhakikisha matokeo ya tafiti zao yanaifikia Jamii wakiwemo wawekezaji na kampuni za kibiashara ili matokeo hayo yatumike kibiashara na kutatua kero mbalimbali kwa jamii.

Wito huo umetolewa leo Februali 20 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli wakati wa hafla ya Makabidhiano ya Ofisi kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya  Utafiti wa Kilimo (TARI)  Dkt. Godfrey Mkamilo anayemaliza muda wake na kumkaribisha  Mkurugenzi Mkuu mpya Dkt. Thomas Bwana, hafla iliyofanyika kwenye Makao Makuu ya TARI - Makutopola Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Mweli amesema, zipo tafiti ambazo matokeo yake yamekuwa yakitoa mwanga katika kukabiliana na kero mbalimbali kwenye jamii ikiwemo sekta ya kilimo huku tafiti nyingine zikiweza kutumiwa na wawekezaji kupata suluhisho kwa changamoto  mbalimbali kwenye masoko.

Alisema, kwa kuwa TARI ina watafiti ambao baadhi ya tafiti zao zimekuwa ni suluhisho kwenye changamoto ya mbegu huku wengine tafiti zao zinaweza kutumika kwenye uongezaji wa thamani za  bidhaa zinazotakiwa sokoni, hivyo ni wakati wa kuingia makubaliano na wawekezaji kwenye sekta binafsi ili kushirikiana kwenye kutumia kibiashara ugunduzi uliotokana na tafiti husika.

Amesema,“zipo tafiti zilizofanywa na watafiti wa TARI hususan katika mbegu, mbolea na hata chakula zenye majibu sahihi yenye kuleta matokeo chanya katika jamii, sasa yapo matokeo ya tafiti ambayo yanaweza kutumika kibiashara na ndiyo muda wa kufanya kazi pamoja na sekta binafsi katika kuhakikisha matokeo hayo ya utafiti yanageuzwa bidhaa sokoni.”

Pia Mweli ameitaka TARI kuvitumia kikamilifu  Vituo vya Umahiri (Centre of Excellence ) vya Wizara ya Kilimo katika kutekeleza majukumu yao ya kitafiti huku akiwahakikishia kuwa Wizara ya Kilimo itahakikisha hapa nchini kunakuwa na vifaa vya kisasa vya utafiti vinavyokidhi vigezo vya kimataifa.

Katika hotuba yake kabla ya kukabidhi ofisi, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt.  Godfrey Mkamilo mbali na kuishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuiwezesha TARI kufanya shughuli zake kiufanisi, amewataka wafanyakazi wa TARI kuendelea kujikita kwenye ubunifu ikiwa pamoja na kufanya kazi kiufanisi ili kutimiza malengo ya Taasisi hiyo.

Amesema,“Wizara ya Kilimo imekuwa ni msaada mkubwa kwa TARI hasa kwa kuhakikisha Taasisi hii inaongezewa bajeti ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi, hivyo niwasihi kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi katika kuendeleza shughuli za Taasisi hii, fanyeni kazi na fanyeni tafiti zenye matokeo.”

Naye Mkurugenzi Mkuu mpya wa TARI, Dkt. Thomas Bwana amewataka wafanyakazi wa TARI kuhakikisha wanatimiza malengo ya Taasisi ili iwe kituo cha umahiri katika tafiti zenye tija na zenye kuleta mageuzi kwenye kilimo.