Skip to main content
Habari na Matukio

TANZANIA KUVUTIA WAWEKEZAJI COP28

Tanzania iko tayari kushiriki katika Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi ujulikanao kama COP28 UAE.

Mkutano huo umeanza tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2023 Dubai, chini ya mwenyeji wake Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo washiriki zaidi ya elfu sabini kutoka nchi takribani 190 wanashiriki.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anaongoza ujumbe wa Tanzania unaohusisha Waheshimiwa Mawaziri akiwemo Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo, Makatibu Wakuu, Mabalozi, Viongozi na Watalaamu kutoka Wizara za Kisekta, Idara za Serikali, Mashirika ya Umma, Vyuo Vikuu, Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia, Vijana na Wanahabari kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Kaulimbiu ya Kitaifa katika Mkutano huo ni “Kuimarisha Kilimo Himilivu na Uchumi wa Bluu katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi”. Lengo la kauli mbiu ni kutoa msisitizo katika matumizi ya teknolojia na mbinu bora zinazozingatia changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ili kuongeza tija katika uzalishaji, mnyororo wa thamani wa mazao na masoko. Vile vile, kauli mbiu inalenga kujenga uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika kukuza uchumi wa kijani na kuchochea maendeleo endelevu.

Mhe. Rais Dkt. Samia anatarajiwa kushiriki na kuhutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali ambapo pamoja na mambo mengine, Tanzania itakuwa na mikutano ya uwili na nchi mbalimbali katika kukuza diplomasia ya uchumi, mikutano ya pembezoni ya masuala ya kilimo na uchumi wa kijani; ikiwa ni pamoja na kuzindua matumizi ya nishati safi ya kupikia na uchumi wa buluu.

Mapinduzi ya kilimo kwa upande wa Tanzania yameleta hamasa kubwa kwa vijana na wanawake nchini Tanzania, hususan kupitia programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (Build a Better Tomorrow – BBT).  Aidha, Tanzania ni moja kati ya nchi 190 zinazoshiriki katika Mkutano wa COP28 na inatarajia kuvutia uwekezaji na biashara katika kuleta maendeleo ya uchumi wa kijani (green growth), ikiwa ni pamoja na sekta nyingine za uchumi nchini.