Skip to main content
Habari na Matukio

TARI UKIRIGURU YAGUNDUA AINA 10 ZA MBEGU BORA ZA PAMBA

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia kituo cha Ukiriguru mkoani Mwanza imefanikiwa kugundua aina kumi za mbegu bora za zao la pamba kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima nchini.

Hayo yamebainishwa leo (30.04.2020) na Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt.Geofrey Mkamilo wakati akiwasilisha ripoti ya utendaji kazi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo alipotembelea kituo hicho wilayani Misungwi.

Aina mpya za mbegu zilizogunduliwa ni pamoja na UK 173,uk 08,UK 171  na UK91. Imeelezwa kuwa mbegu hizo zina uwezo wa kutoa mavuno tani 2.5 hadi 3.0 kwa hekta na kuwa na zinahimili ukinzani wa mnyauko fuzari.

Akizungumzia mafanikio hayo Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo alisema wizara inataka kuona mbegu hizo bora zinafikishwa kwa wakulima wote kwenye mikoa 17 inayozalisha pamba nchini.

Aliongeza kusema watafiti wa mbegu bora wanapaswa kuendelea kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais Dkt.John  Pombe Magufuli  la kuzalisha mbegu nyingi za pamba na mazao mengine ili nchi ijitosheleze kwa mbegu.

“ Mikoa 17 nchini inalima zao la pamba na inataka mbegu bora toka Ukiriguru.Tunahijati mzalishe mbegu nyingi zaidi na kusambaza kwa wakulima kwa wakati” alisisitiza Kusaya

Takwimu za uzalishaji pamba msimu wa 2019 ilikuwa tani 348,910  kati ya lengo tani 450,000 ambazo ziliuzwa kupitia vyama vya ushirika(AMCOS) na kuingiza shilingi Bilioni 419.

TARI Ukiriguru imefanikiwa pia kugundua aina  16 za mbegu za mihogo aina ya Mkumba,Mkuranga 1,Kizimbani,Kiroba,TARICASSA1,2,3,4 na TARICASS 5 zenye uwezo wa  kutoa mavuno  mengi tani  20 hadi 40 kwa hektari na zenye ukinzani wa magonjwa ya CMD na CBSD.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo ameviagiza Vyuo vya mafunzo ya kilimo nchini  kuanzisha mashamba darasa  bora ya mazao ili wazalishe na kuuza kwa wakulima lengo ikiwa vijiendesha kibiashara.

Akizungumza na watumishi wa Chuo cha Kilimo ( MATI) Ukiruguru, Katibu Mkuu huyo alisema uwepo wa maeneo makubwa ya ardhi kwenye vyuo vya mafunzo utumike kuzalisha mazao mengi ya aina tofauti  na kuuza kwenye masoko.

“ Nataka tuone namna vyuo vyetu vitaendeshwa kibiashara kwani uwezo tunao na utaalam upo .Kama mnaweza kufundisha vijana kilimo cha kisasa na ufugaji kwanini msianzishe kilimobiashara hapa na kujiongezea kipato ? alihoji Katibu Mkuu

Katibu Mkuu huyo amesema wizara inazo taasisi za utafiti wa mazao kama TARI na ASA ambazo zinajukumu la kuzalisha mbegu ,hivyo vyuo vifanye utaratibu kuanzisha mashamba ya kilimo biashara

Kusaya ameahidi kupatia chuo cha MATI Ukiruguru trekta moja na kompyuta kumi (10) ili kusaidia utendaji kazi wa chuo hicho na kuongeza kuwa kuanzia sasa watumishi wote watalipwa stahili za posho ya masaa ya ziada toka wizarani ili kuinua ari na motisha ya kufanya kazi kwa watumishi.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Frenk Onesmo alisema wanaendelea na mafunzo ya vijana katika fani za kilimo na sasa wameanza kufundisha kilimo cha mazao kama alizeti,mdarasini na mbogamboga ili kuwajengea uwezo.

Mwisho.

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

MWANZA

30.04.2020